Tuesday 19 November 2013

Mashauri ya rufani kutolewa uamuzi


Na Mary Gwera wa Mahakama ya Tanzania
MASHAURI 188 yanatarajiwa kusikilizwa na kutolewa uamuzi katika kipindi cha Novemba na Desemba, kutokana na vikao vya Mahakama ya Rufani vilivyoanza rasmi wiki hii.
Vikao hivyo vimeanza rasmi katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mwanza na Zanzibar, ambapo kikao chake kitaanza rasmi Desemba 2, mwaka huu.
Kaimu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Zahra Maruma, aliyasema hayo kupitia taarifa yake kuhusu vikao hivyo vya mahakama hiyo.
Alisema miongoni mwa mashauri ambayo yatasikilizwa yanahusisha mashauri ya rufani za jinai, madai na maombi mbalimbali ya rufani hizo.
Zahra alisema katika mkoa wa Arusha, rufani  45 zitasikilizwa na kutolewa uamuzi mbele ya jopo la majaji watatu wakiongozwa na Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande.
Majaji wengine watakaosikiliza mashauri hayo ambayo 35 ni ya jinai na 10 ya maombi ya madai ni Nathalia Kimaro, Bernard Luanda na Jaji Bethuel Mmila.
Kwa upande wa Dar es Salaam, mashauri 81 yamepangwa kufanyiwa kazi na yatasikilizwa na majaji tofauti, kulingana na idadi ya kesi akizopangiwa kila mmoja.
Zahra aliwataja majaji wataosikiliza kesi katika mkoa huo kuwa Jaji Engela Kileo, Jaji  Sauda Mjasiri, Jaji William Mandia, Jaji Mbarouk Mbarouk na Jaji Stephen Bwana.
Alisema kwa upande wa Mwanza, mashauri 44 yatasikilizwa chini ya jopo la majaji watatu, likiongozwa na Jaji Edward Rutakangwa, Jaji Semistocles Kaijage na Jaji Kipenka Mussa.
Kaimu msajili huyo alisema kikao kingine kinatarajia kufanyika Zanzibar Desemba 2, mwaka huu, ambapo mashauri 18 yakiwa ni rufani za jinai na madai yatasikilizwa na kutolewa uamuzi katika kikao hicho.
Alisema katika kikao hicho kitakachofanyika visiwani Zanzibar, kitakuwa na jopo la majaji watatu likiongozwa na Jaji Mbarouk, Jaji Luanda na Jaji Ibrahim Juma.
Zahra alisema vikao  hivyo vyote vitakamilika rasmi Desemba 13, mwaka huu na hivyo alitoa wito kwa wahusika kutoa ushirikiano ili kuweza kufanikisha kazi hiyo muhimu.
Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu nchini zimejiwekea utaratibu wa kusikiliza mashauri katika mikoa mbalimbali, lengo likiwemo  kupunguza idadi ya mashauri katika mahakama hizo.  Hali hiyo, inalenga pia katika kupunguza mlundikano wa kesi mahakamani.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru