Wednesday, 20 November 2013

Kitanzi chamgeukia Waziri Dk. Mgimwa


NA SULEIMAN JONGO, PERAMIHO
WAZIRI wa Fedha, Dk. William Mgimwa ni miongoni mwa mawaziri watakaoitwa kwenye kikao cha Kamati Kuu ya CCM, kwa ajili ya kuhojiwa kutokana na uchelewashaji wa fedha za malipo ya wakulima wa mahindi.
Akiwahutubia wananchi wa kijiji cha Masangu, Kata ya Magagula wilaya ya Songea mkoani Ruvuma, Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema, Waziri wa Fedha ndiye mwenye dhamana ya fedha zote za serikali.
Kinana alisema waziri huyo hawezi kuachwa, huku wakulima na wadau wa mazao ya mahindi wakiwemo waliosafirisha wakiwa hawajalipwa fedha zao.
“Ninachokisimamia ni maagizo ya Mkutano Mkuu wa Nane ulioagiza Chama kusimamia serikali zake mbili ya Muungano na ile ya Mapinduzi Zanzibar. Hivyo sifanyi mimi binafsi,” alisema.
Alisema waziri huyo lazima aitwe na kuhojiwa katika kikao cha Kamati Kuu ya CCM kitakayofanyika mwezi ujao mjini Dodoma.
Kinana alimtaka Dk. Mgimwa kujiandaa na mambo manne, ikiwemo kujibu hoja kuwa kwa nini wakulima wa mahindi hawakulipwa fedha zao baada ya kuuuza kwenye ghala la taifa.
Swali la pili ni kwa nini fedha za pembejeo hazilipwi kwa wakati, huku zikiwa tayari zimeshatengwa kwenye bajeti ya serikali.
Alitaja hoja nyingine anayopaswa kujiandaa kuijibu ni kwa nini bajeti ya serikali ilichelewa kutekelezwa, licha ya kusomwa Aprili badala ya Julai kwa lengo la kuanza kutekelezwa mapema.
Kinana alitaja hoja ya mwisho kuwa kwa nini kumekuwa na malalamiko mengi kutoka kila eneo, ikiwemo serikalini kuhusu ucheleweshaji fedha za kutekeleza shughuli mbalimbali.
“Haiwezekani wakuu wa wilaya, wakurugenzi na watendaji wa serikali wote walalamike kutopatikana fedha wakati zilishaidhinishwa. Viongozi wote walipoteuliwa kushika nafasi mbalimbali hawakukataa, bali walifurahi na kuahidi kuwahudumia wananchi, hivyo hilo ndilo tunalolisubiri na kulitarajia,” alisema.
Wakati huo huo, Dustan Ndunguru anaripoti kuwa, CCM imesema wakati umefika kwa serikali kuangalia upya utaratibu wa kununua mazao ya wakulima, ambapo inapaswa inunue kwa fedha taslimu badala ya kuwakopa.
Kutokana na hilo, kimetaka serikali kupitia Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika kuwalipa wakulima wa mahindi fedha zao wanazodai baada ya kuuza mazao yao kwa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ili wapate uwezo wa kugharimia mashamba waliyoyaandaa kwa ajili ya msimu ujao wa kilimo.
Kinana alitoa mapendekezo hayo alipokuwa akihutubia mkutano huo, ambapo alisema kimsingi watendaji na viongozi waliopewa dhamana ya kusimamia kilimo hapa nchini hawatekelezi majukumu yao kwa umakini na kutokana na hali hiyo, wazalishaji wa mazao kama korosho, tumbaku na mahindi wamejikuta wakikosa mtetezi wa dhati, hivyo kuibua manungíuniko.
Alisema CCM ndiyo iliyopewa ridhaa na wananchi ya kuunda dola, hivyo ina wajibu wa kupambana na wavivu, wazembe ambao wamepewa dhamana ya kuwatumikia wananchi, kwani wamekuwa wakilipwa mishahara kwa kodi za Watanzania na kuwa walichotakiwa kufanya ni kutekeleza majukumu yao kwa ufasaha.
Katika hatua nyingine, Kinana alishangazwa na taarifa zilizotolewa na wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM wilayani hapa kuwa baada ya serikali kubadili mfumo wa utoaji wa pembejeo za ruzuku kwa vikundi, sasa hali hiyo imebadilishwa na kuwapa jukumu mawakala ambao kwa muda mrefu wamekuwa sio waaminifu.
Mbunge wa Peramiho, Jenista Mhagama, alisema wakulima wengi walihamasika kujiunga na kuanzisha vikundi kwa malengo ya kupata pembejeo hizo, lakini wamekatishwa tamaa na kitendo cha jukumu hilo kwa asilimia 20 kuwapa vikundi, huku mawakala wakipewa jukumu la kusambaza pembejeo hizo kwa asilimia 80.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru