Na mwandishi wetu, zanzibar
RAIS wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Sheni, ameitaka Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuimarisha utafiti kwa kuwa majukumu ya msingi ya wizara hiyo yanategemea zaidi utafiti.
Hivyo, alisema Wizara haina budi kuzingatia hilo pindi ipangapo bajeti yake kwa kuzipa kipaumbele kazi za utafiti ili kuleta uwiano wa vipaumbele katika mipango ya wizara.
Aliitaka Idara ya Mipango, Sera na Utafiti katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kuchangamkia masuala ya utafiti hata kama ni kwa kuwashajiisha watafiti kutoka nje ya wizara.
Dk. Sheni aliyasema hayo alipokuwa akihitimisha kikao cha Kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango kazi wa wizara hiyo kwa mwaka 2012/2013, jana.
Aliikumbusha kuendeleza ushirikiano wa karibu pia na Wizara ya Biashara, Viwanda na Masoko, katika kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei ndogo ya zao la mwani.
Alisema limekuwa jambo jema kwa wananchi kuitikia wito wa serikali wa kuendeleza kilimo cha mwani ambacho kinaifanya Zanzibar sasa kuwa nchi ya pili duniani kwa uzalishaji wa zao hilo.
“Ni lazima jitihada zifanywe kulitafutia ufumbuzi tatizo la bei kabla ya wananchi hawajakata tama,” alisema Dk. Sheni.
Akitoa maelezo ya awali ya Wizara katika kikao hicho, Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdillah Jihad Hassan, alisema wizara kwa kipindi cha mwaka wa fedha 2012/2013 iliweza kutekeleza malengo yake kwa ufanisi kwa asilimia 64.
Alisema Idara ya Mipango, Sera na Utafiti, ilitekeleza malengo yake kwa asilimia 72, Idara ya Uendeshaji na Utumishi asilimia 81, Idara ya Huduma za Utabibu wa Mifugo asilimia 59, Idara ya Uzalishaji Mifugo asilimia 77, Idara ya Maendeleo ya Uvuvi asilimia 47 na Idara ya Mazao ya Bahari asilimia 85.
Alisema katika kipindi hicho, Wizara ilitoa huduma mbalimbali kwa walengwa ili kuimarisha maendeleo ya mifugo na uvuvi nchini.
Alisema wastani wa wafugaji 34,000, wavuvi 38,000, wazalishaji wa mwani 21,000 na vikundi 146 vya wafugaji wa mazao ya baharini, walifaidika na huduma hizo.
Waziri huyo, alikieleza kikao hicho kuwa sekta ya mifugo ilikuwa kwa asilimia 3.1 na kuchangia asilimia 4.2 ya pato la taifa mwaka jana, huku sekta ya uvuvi ilikuwa kwa asilimia 2.3 na kuongeza mchango wake kwa pato la taifa kutoka asilimia 6.7 mwaka 2011 hadi asilimia 7.1 mwaka jana.
Sekta ya uvuvi imezidi kuimarika kutokana na kuongezeka kwa uvuvi wa baharini na ufugaji wa samaki na mazao ya baharini.
Ilielezwa kuwa jumla ya tani 9.7 za samaki waliovuliwa kutoka katika mabwawa ya wananchi mwaka jana.
Tani 7.7 zilivuliwa Pemba ikilinganishwa na tani 2.0 katika kisiwa cha Unguja.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru