Wednesday 27 November 2013

Mgomo mpya wanukia TRL


NA MWANDISHI WETU
MGOMO mwingine unanukia katika Shirika la Reli Tanzania, safari hii ukiwahusisha askari wanaolinda usalama wa abiria pindi wawapo safarini.
Askari hao wanadai kutolipwa posho za safari kwa zaidi ya mwaka mmoja, wanadai kila wanapoubana uongozi ili uwalipe, hupigwa danadana.
Habari za kuaminika zinadai kuwa baadhi ya askari hao wanajipanga kuingia kwenye mgomo wa kutotoa huduma za ulinzi kama njia ya kushinikiza kulipwa.
Ilielezwa kuwa askari hao ambao hufanya doria ya ulinzi wakati wa safari za treni, hulipwa posho za safari kwa ajili ya kujikimu lakini tangu Novemba, mwaka jana, hawajalipwa.
Hatua hiyo inadaiwa kuwa inaweza kusababisha askari hao kusafirisha abiria kinyume cha utaratibu kwa lengo la kujipatia kipato.
“Inafikia wakati mtu unakosa hata fedha ya kujikimu njiani, jambo hili ni la hatari kwa sababu mtu unalazimika kuwa omba omba na familia zetu hazituelewi kabisa,’’ kilisema chanzo chetu.
Chanzo hicho, kilidai kuwa askari wa nchi nzima walifikisha malalamiko yao katika ngazi husika na tangu wakati huo, walielezwa madai yao yanashughulikiwa.
Akizungumza kwa njia ya simu na Uhuru jana, Kamanda wa Kikosi cha Reli, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Saada Haji, alithibitisha kuwepo kwa madai hayo na kuwa bado yanashughulikiwa.
Pia, aliwataka askari kufuata sheria na utaratibu wa kazi yao katika masuala mbalimbali hasa wanapokuwa na madai na si kukimbilia katika vyombo vya habari.
“Masuala yao yanashughulikiwa, ni kweli wanalidai Shirika la Reli na hata kama wanamadai, wanapaswa kufuata utaratibu wa kudai kwa mujibu wa kanuni na sheria za kazi yao kwani zipo,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru