Thursday 28 November 2013

Luhanjo awaasa viongozi


NA FRANK KIBIKI, NJOMBE
VIONGOZI wa serikali na vyama vya siasa nchini, wametakiwa kutumia nafasi zao kuhakikisha wanashirikiana na wananchi, kujiletea maendeleo kwenye kila ngazi ili kuondokana na umaskini.
Wito huo ulitolewa na Katibu Mkuu Kiongozi mstaafu, Philemon Luhanjo, wakati wa Ibada ya shukrani na kumbukumbu ya kifo cha Waziri wa zamani wa Elimu, na aliyewahi kuwa Mbunge wa jimbo la Njombe Kaskazini, Jackson Makweta, iliyofanyika nyumbani kwake, Kijiji cha Hagafilo, mkoani Njombe.
Alisema kama ilivyokuwa kwa Makweta, kila kiongozi atumie nafasi yake kuhakikisha anasaidiana na wananchi katika kujiletea maendeleo.
Luhanjo, alisema ni vyema kwa viongozi kujua wanaacha alama gani kwa jamii wanayoongoza kama mchango wao kwa maendeleo.
Huku akimtolea mfano wa Makweta, katika kuboresha sekta ya elimu mkoani Njombe, alianzisha shule za wazazi kwa kila tarafa ambazo zilikuwa zikiitwa Njombe District Development Trust (NDDT).
Zililenga kuwasaidia wanafunzi wanaokosa nafasi ya kujiunga na shule za sekondari za serikali.
“Makweta ameacha historia na alitumia talanta zake kama kiongozi kusukuma maendeleo na wananjombe, tutamkumbuka daima, ni vyema viongozi wa sasa waige mfano wake,” alisema Luhanjo.
Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Kapteni Aseri Msangi, alisema kiongozi huyo aliacha pengo kubwa mkoani humo na aliahidi kuiga mfano wake.
Wakitoa maoni yao, wakazi wa Njombe, waliwashauri viongozi wasio na maadili na uwezo wa kuchapa kazi, wawapishe wenye uwezo.
Naye mjane wa marehemu, Twihuvila Makweta, alitumia fursa hiyo kuishukuru serikali na watu waliokuwa pamoja wakati wote wa maombolezo na msiba wa mume wake.


Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru