Wednesday, 30 July 2014

Maafa makubwa  • Ajali basi na lori yaua 17, yajeruhi 56
  • Waliokufa, waliojeruhiwa watambuliwa
  •  DC Kangoye aongoza shughuli ya ukoaji

Na Waandishi Wetu
WAKATI Waislamu wakiendelea kusherehekea Sikukuu ya Idd elFitri, vilio na simanzi vimetawala eneo la Pandambili wilayani Kongwa, Dodoma, kutokana na ajali mbaya iliyosababisha watu 17 kupoteza maisha.


Mbali na vifo hivyo, ajali hiyo iliyohusisha basi la Kampuni ya Moro Best na lori lililokuwa limebeba mabomba, pia imejeruhi watu wengine 56. Katika ajali hiyo madereva wote wa basi na lori pamoja na wasaidizi wao, wamepoteza maisha.
Mkuu wa Wilaya ya Mpwapwa, Christopher Kangoye, ambaye alifika eneo la tukio muda mfupi baada ya ajali, alisema ilihusisha basi hilo lenye namba T 258 AHV aina ya Scania, ambalo liligongana uso kwa uso na lori lenye namba T 820 CKU likiwa na tela lake.
Alisema lori hilo lililokuwa limepakia mabomba, liligongana uso kwa uso na basi na kwamba chanzo ni uzembe wa dereva wa lori.
Alisema dereva huyo alikuwa akijaribu kulipita gari bila kuchukua tahadhari. Kabla  ya kugongana uso kwa uso na basi, aligonga gari lingine.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, alisema ajali hiyo ilitokea jana saa mbili asubuhi na kati ya waliopoteza maisha 12 ni wanaume na wanawake ni watano.
Alisema basi hilo lilikuwa likitoka Mpwapwa kwenda Dar es Salaam na lilikuwa likiendeshwa na Said Lusogo huku lori likiendeshwa na Gilbert Nemanya.
Kamanda Misime alisema mpaka jana jioni, miili ya watu 11 ilikuwa imetambuliwa na ndugu na jamaa.
Waliotambuliwa ni dereva wa lori Gilbert Nemanya na utingo wake Mikidadi Zuberi, dereva wa basi la Morobest, Saidi Lusogo na kondakta wake, Omary Mkubwa.
Wengine ni Merina Malikeli, Nasib Machenje, Wilson Suda, Gabriel Mejachiwipe, Justine Makasi na mwanamke aliyetambuliwa kwa jina la Christina.
Kamanda Misime alisema majeruhi 56 wa ajali hiyo wamelazwa Hospitali za Wilaya ya Kongwa na Hospitali ya Rufani ya Mkoa wa Dodoma, ambapo wamepata majeraha mbalimbali mwilini.
Mpaka jioni, majeruhi waliokuwa wamelazwa Dodoma walikuwa 23 wakiwemo Frank Raymond, Patricia Ngamwai, Amos Chiwaga, Mary Mateo, Safari Jonas, Suzan Charles, Gasper Shao, Felician Rite, Felister Mathias, Amos Jonas, Edina Lwande, Seleman Kaseni, Nazareth Kasua, Simon Msoloka, Juma Mtezi na Swalehe Bakari.
Wengine ni Naseria John, Getruba Kombo, George Njelewa, Manase Makuja, Chibago Mchiwa, Nicholous Roger na Michael Chibwela.
Kangoye aliwataka wananchi wenye ndugu na jamaa waliokuwa wakisafiri na basi hilo, kufika kwenye hospitali kwa ajili ya kuwatambua.
Eneo la Pandambili limekuwa maarufu kutokana na ajali za mara kwa mara zinazogharimu maisha ya watu. Ni eneo ambalo aliyekuwa Mbunge wa Tarime, Chacha Wangwe, alipata ajali mbaya na kufariki dunia papo hapo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru