Na Mwandishi Wetu
RAIS Jakaya Kikwete amesema Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), umeisaidia Tanzania kutatua changamoto za maendeleo, ikiwemo ujenzi wa miundombinu na kuimarisha sekta ya afya.
Akizungumza wakati wa mkutano na waandishi wa habari kati yake na Rais wa Marekani, Barack Obama, Ikulu, Dar es Salaam jana, alisema miradi hiyo imekuwa na tofauti kubwa ikilinganishwa na misaada ya wahisani wengine.
Rais Kikwete alisema miradi hiyo inatoa fursa kwa nchi kujichangulia vipaumbele vyake, na kuwekeza tofauti na misaada kutoka nchi zingine wahisani.
Alisema kupitia MCC Tanzania imeweza kujenga miundombinu ya barabara, ambayo awali ilikuwa ni changamoto kubwa katika baadhi ya mikoa, ikiwemo Ruvuma na Mtwara.
Kwa mujibu wa Rais Kikwete, kupitia fedha za MCC, Tanzania imejenga barabara mbalimbali, zikiwemo za Namtumbo, Mbinga, Horohoro, Tunduma na Pemba, ambazo zilikuwa vipaumbele vya taifa
Barabara nyingine alisema ni za mikoa ya Rukwa na Mbeya.
Rais alisema mradi mwingine ni wa maji wa Dar es Salaam, ambao umetekelezwa kupitia MCC.
Alisema kupitia fedha za MCC, Tanzania imepunguza maambukizi ya malaria kwa asilimia 50, vifo vya watoto na maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.
MCC pia umeinufaisha Tanzana katika elimu, ambapo hivi sasa kila mtoto ana kitabu cha sayansi na hesabu tofauti na ilivyokuwa awali, ambapo kitabu kimoja kilitumika kwa watoto watano.
“MCC imetusaidia kupunguza vifo vya wajawazito na watoto, maambukizi ya VVU na maambukizi ya malaria, mambo ambayo yalikuwa yakiathiri ustawi wa jamii,” alisema.
Akizungumzia ujio wa viongozi wa kimataifa, Rais Kikwete alisema hiyo ni neema na ishara ya kufanya vizuri kwa Tanzania katika mambo mbalimbali.
Rais alisema Tanzania itaendeleza amani na utulivu ili kuwa kichocheo cha maendeleo.
Monday, 1 July 2013
Misaada ya MCC imeiinua Tanzania
10:22
No comments
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru