Monday, 1 July 2013

Michelle atembelea Makumbusho



NA SELINA WILSON
MKE wa Rais wa Marekani, Michelle Obama, ametembelea Makumbusho ya Taifa, jijini Dar es Salaam, na kuweka shada la maua katika eneo yalikohifadhiwa mabaki ya mlipuko wa bomu katika ubalozi wake nchini.
Michelle alikwenda eneo hilo akifuatana na mke wa Rais Mama Salma Kikwete.
Katika mlipuko uliotokea kwenye ubalozi wa Marekani nchini, Agosti 7, 1998, watu 11 walipoteza maisha na wengine kadhaa walijeruhiwa, huku mali zikiteketea.
Mama Salma na mgeni wake waliwasili katika eneo hilo jana, saa 10.30 jioni.
Katika eneo hilo kuna mabaki ya pikipiki, baiskeli na magari, likiwemo gari la ubalozi huo lenye namba ya usajili T 116 CD 639.
Pia kuna orodha ya majina ya watu 11 waliopoteza maisha katika tukio hilo.
Orodha hiyo iliwekwa na aliyekuwa Balozi wa Marekani wakati huo, Charles Stith.
Majina hayo ni ya Abdulrahman Abdallah, Paul Elisha, Ramadhan Mahundi, Abbas Mwilla, Yusuf Ndage, Bakar Nyumbu, Mtendeje Rajabu, Dotto Ramadhani, Rogath Said, Hasaan Siad na Aimosari Mzee.
Mlipuko huo ulitokea sambamba na mwingine katika ubalozi wa nchi hiyo Kenya, ambako watu 44 walipoteza maisha, kati yao 12 wakiwa raia wa Marekani na wafanyakazi wengine 32 wa ubalozi huo.
Wake hao wa marais walifuatana na wanafunzi Halima Haji na Domina Maile wa Shule ya Sekondari WAMA Nakayama, waliobeba mashada ya maua.
Mama Salma alimuongoza Michelle kuweka shada na baadaye kwenda kwenye ukumbi wa Makumbusho ya Taifa kuangalia burudani.
Michelle alifuatana na wanawe Malia na Sasha, huku Mama  Salma akiwa na wanawe Mwanaasha na Rashid.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru