Na Suleiman Jongo
RAIS Barack Obama wa Marekani, amemmwagia sifa Rais Jakaya Kikwete, kwa kusimamia demokrasia barani Afrika.
Pia amempongeza kwa matumizi mazuri ya misaada ya Marekani inayotolewa kwa Tanzania.
Rais Obama aliyewasili nchini jana, amesema amekuwa akivutiwa na jinsi Tanzania chini ya uongozi wa Rais Kikwete inavyotumia vyema misaada ya Marekani, ikiwemo inayotolewa kupitia Mfuko wa Changamoto za Milenia (MCC), hivyo kuimarisha uchumi.
Alitoa pongezi hizo katika mkutano na waandishi wa habari uliomuhusisha pia Rais Kikwete, uliofanyika kwenye viwanja vya Ikulu, mjini Dar es Salaam.
Tanzania na Marekani zina miradi mbalimbali ya ushirikiano wa kimaendeleo, ambayo imekuwa na manufaa kwa wananchi, ikiwemo ya MCC, inayolenga kuboresha baadhi ya maeneo yanayohusu maisha ya Watanzania.
Mradi mwingine ni wa AGOA, ambao ni mahsusi kwa ajili ya soko nafuu la bidhaa kutoka Tanzania kwenda Marekani.
Kwa mujibu wa Rais Obama, kutokana na mafanikio hayo, Tanzania ni miongoni mwa nchi nne zitakazonufaika na awamu ya pili ya miradi ya MCC.
Alisema kutokana na kuvutiwa huko, Marekani imepanga kuisaidia zaidi Tanzania ili kujiimarisha, isiwe katika kupokea misaada tu, bali kuzalisha na kufanya biashara.
Rais Obama alimpongeza Rais Kikwete na Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohammed Sheni, kwa ujenzi wa taasisi za kiserikali na kuimarisha demokrasia, ambayo imekuwa kichocheo cha utulivu na ukuaji uchumi.
Alieleza kufurahishwa na kazi nzuri inayofanywa na Rais Kikwete katika kushughulikia migogoro katika nchi za Maziwa Makuu, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Obama akizungumzia suala la DRC, alisema chanzo ni utajiri uliopo ndani ya ardhi ya nchi hiyo na kwamba, mgogoro huo utatatulia kwa nchi jirani kuheshimu mikataba ya amani iliyofikiwa.
Alisema iwapo nchi jirani zitashirikiana kuhakikisha DRC inakuwa na amani, mataifa hayo nayo yatanufaika kwa kufanya biashara, hivyo kukuza uchumi.
Kuna Maoni 0 mpaka sasa.
Toa Maoni Yako Kwa Uhuru