Wednesday 14 May 2014

Bajeti ya Zanzibar 2014/2015 hadharani


na Mwandishi Wetu, Zanzibar
SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), imetangaza bajeti kwa mwaka wa fedha 2014/2015, ambapo mkazo umewekwa katika ukusanyaji wa kodi na utekelezwaji wa miradi ya maendeleo na kupunguza umasikini.
Bajeti hiyo iliwasilishwa jana na Waziri wa Fedha, Omary Yusuph Mzee, ambapo aliwaeleza Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi kuwa, katika bajeti ya mwaka 2014/2015, SMZ inatarajiwa kukusanya sh. Bilioni 707.8 ikiwa ni ongezeko la asilimia 7.5 ya Makadirio ya Bajeti ya mwaka 2013-2014.
Alisema sh. bilioni 365.8 zinatarajiwa kukusanywa katika mapato ya ndani katika mwaka 2014/2015, ukilinganisha na mapato ya mwaka 2012/2013 ya sh. bilioni 326.
Alisema serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka mikakati ya kukusanya mapato zaidi katika vianzio vyake mbali mbali kupitia taasisi zake za kukusanya mapato.
Mzee, alisema Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), inakadiriwa kukusanya jumla ya sh. bilioni 166.1 sawa na asilimia 25.7 ya mapato halisi yaliyokusanywa katika mwaka 2013/2014 ya sh.bilioni 132.1.
Aidha, Waziri Mzee, aliwaambiya wajumbe wa Baraza hilo kwamba, mishahara ya watumishi wa SMZ itachukuwa asilimia 55.2 ya mapato yote yanayokusanywa na serikali.
Alisema serikali ya SMZ haitarajii kuongeza mishahara ya watumishi wake, isipokuwa itafanya marekebisho ya mishahara kwa kada mbali mbali.
Mzee, alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2014/2015, serikali itaongeza ada ya usalama wa anga kwa ajili ya kuimarisha mamlaka ya viwanja vya ndege nchini (ZAA).
Aidha, alisema mamlaka mbili zinazokusanya mapato nchini ZRB na TRA, zipo katika mchakato wa kuwatambua walipa kodi wote ili kubaini kama wanalipa mapato ipasavyo katika taasisi husika.
Katika mwaka wa fedha 2014/2015, serikali inatajiwa kutumia jumla ya sh.bilioni 707.8, kati ya fedha hizo, matumizi ya kawaida ni sh. bilioni 376.5 na sh. bilioni 331.3 ni kwa ajili ya mpango wa maendeleo.
Alisema katika bajeti hiyo, mkazo umewekwa katika kuimarisha Mpango wa Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) na dira ya maendeleo ya mwaka 2020 na ilani ya uchaguzi mkuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2014.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru