Wednesday 28 May 2014

CHADEMA ‘inatumika’ na Rwanda - Membe


NA ABDALLAH MWERI
SERIKALI imesema itachukua hatua kali kwa baadhi ya Watanzania, ambao watabainika kutoa siri za nchi kwa ajili ya manufaa binafsi.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe, alipokuwa akijibu hotuba ya Kambi ya Upinzini iliyosomwa na Mbunge Ezekiel Wenje (Nyamagana-CHADEMA).
Katika hotuba yake, Wenje ambaye ni Waziri Kivuli wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, alidai kuwa Membe, anachochea vita kati ya Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Membe alisema ni aibu kwa mbunge kusimama ndani ya bunge kutetea maslahi ya Rwanda na kuonya kuwa hatua hiyo ni hatari kwa mustakabali wa nchi.
Alisema ameshangazwa na kauli ya Wenje kwamba Serikali ya Tanzania inaibeba DRC katika vita kati ya nchi hiyo na Rwanda.
Akionekana kukerwa na kauli ya Wenje, Membe alisema mbunge huyo hana nia njema na mustakabali wa wananchi wa Tanzania na lengo lake ni kutaka kuchochea mgogoro kati ya Tanzania na Rwanda.
“Ni aibu kwa Mbunge Wenje kusimama bungeni macho yamemtoka, akiitetea Rwanda. Mtu wa aina hii ni msaliti mkubwa na hafai kuwa kiongozi
“Kwa nini Wenje anatetea nchi jirani? Mtu makini ni lazima apiganie nchi yake hata kama serikali yake inafanya mabaya au mazuri. Mtu wa aina hii ni rahisi kutumika au kutoa siri za nchi,” alisema Membe.
Membe alisema haamini kama kauli ya Wenje ni azimio la chama chake cha CHADEMA na alishangaa kwa nini Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe, ameruhusu hotuba hiyo kusomwa bungeni.
“Mheshimiwa Mbowe ulikuwa wapi mchana wakati kauli za namna hii zilizojaa uchochezi zinasemwa na mbunge wako. Hii ni aibu na nimesikitika sana, naomba Watanzania wafahamu kwamba askari wa M23 ni Wanyarwanda,” alihoji Membe.
Katika kauli yake, Wenje alitetea akidai kuwa askari wa kundi la M23 walioko DRC si raia wa Rwanda, kauli ambayo ilimshitua Waziri Membe.
Waziri huyo alisema yuko tayari kujiuzulu nafasi yake ya uwaziri, ikiwa itathibitika kuwa askari wa 23 si raia kutoka Rwanda.
Pia alimtaka Wenje athibitishe kauli yake kwamba askari hao si raia wa Rwanda na akishindwa, achukuwe hatua ya kujiuzulu nafasi yake ya ubunge.
Mbowe alikiri baadaye kuwa, hotuba iliyotolewa na Wenje ni ya kambi rasmi ya upinzani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru