Sunday 25 May 2014

Nkamia aimwagisa sifa Steps Solar

CHARLES MGANGA
NAIBU Waziri wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Juma Nkamia ameimwagia sifa kampuni ya Steps Solar kwa mkakati wake wa kuwapa huduma ya nishati nuru wananchi wa kipato kidogo nchini.

Akizungumza mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, Nkamia alisema, tayari kampuni hiyo kwa kushirikiana na jamii, imefunga bidhaa zake za nishati ya mwanga katika maeneo mbalimbali wilaya ya Chemba, mkoani Dodoma.

Nkamia alitaja maeneo ambayo kampuni hiyo imetoa vifaa hivyo kwa ajili ya nishati ya mwanga kuwa ni pamoja na shule ya sekondari za Ovada na Kingale  na vituo vya afya vya Tandala na Itolwa.
 

Kimsingi naishukuru kampuni ya Steps Solar kwa kunikabidhi vifaa hivi kwa ajili ya nishati hii ya mwanga. Nina uhakika wanafunzi katika shule hizo watapata fursa ya kujisomea kwa wakati wanaotaka. Pia wagonjwa nao watahudumiwa vyema katika vituo hivyo vya afya ambavyo kampuni hiyo imepeleka nishati hiyo,î alisema Nkamia.

Nkamia ambaye ni mbunge wa Kondoa Kusini alisema, aliwasilisha maombi ya kupatiwa huduma hiyo kabla hajateuliwa kuwa Naibu Waziri.
 

Jamani, msaada huu kwa ajili ya hizi shule na vituo vya afya, niliomba kabla hata ya kuteuliwa kuwa naibu waziri," alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji Dilesh Solanki alisema, lengo la kuanzisha kampuni hiyo ni kuona idadi kubwa ya watu wanaoishi hasa maeneo ya vijijini wakitumia nishati nuru.

Alisema, kwa sababu watu wengi hawajanufaika na huduma hiyo, kampuni yake imeanzisha nishati nuru kwa kushirikiana na serikali katika jitihada za kuhakikisha nishati nuru iliyo na gharama nafuu inasambaa nchini kote.

Alitaja baadhi ya maeneo ambayo mpaka sasa yamenufaika na nishati hiyo ni vituo vya polisi Mjimwema na Feri, vituo vya afya Mjimwema, Ungindani vyote vya Kigamboni jijini Dar es Salaam.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru