Wednesday 14 May 2014

Dengue yapiga hodi Arusha



  • Wauguzi Mount Meru waingiwa hofu, wamsusa mgonjwa 

NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
HOMA hatari ya Dengue imeanza kusambaa katika mikoa mingine nchini, ambapo sasa imevamia jiji la Arusha.
Dengue, ambayo imeshaua zaidi ya watu watano mpaka sasa na wengine zaidi ya 450 wakiendelea kupatiwa matibabu katika Jiji la Dar es Salaam, imezidi kuibua hofu kwa wananchi.
Tayari mkazi wa Maji ya Chai mkoani Arusha, Frank Nnko (30), amelazwa katika Hospitali ya Mkoa wa Arusha ya Mount Meru, akitokea Hospitali ya Wilaya ya Meru (Patandi).
Hata hivyo, wakati Nnko akifikishwa hospitali hapo, hali haikuwa shwari kutokana na baadhi ya wauguzi kushindwa kumpatia huduma kwa wakati kwa kile walichodai kuogopa kuambukizwa.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, Nnko alilazimika kusubiri kwa saa mbili akiwa kwenye gari la wagonjwa lililomfikisha hospitalini hapo kusubiri wapate vifaa vya kujikinga na ugonjwa huo.
Hatua hiyo ilisababisha ndugu na jamaa wa mgonjwa huyo kulalamikia hatua hiyo huku wakihoji iwapo ni kweli serikali imesambaza vifaa tiba vya kukabiliana na ugonjwa huo.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, John Mongela, alithibitisha kuwepo kwa mgonjwa huyo na kuongeza kuwa tayari ameanza kupatiwa matibabu ikiwa ni pamoja na vipimo.
Alisema vipimo vya mgonjwa huyo vimeletwa jijini Dar es Salaam kwa ajili ya uthibitisho zaidi.
Mongela alisema mgonjwa huyo alifikishwa hospitalini hapo jana saa 10 jioni, ambapo baada ya msuguano mkali wa wauguzi kukwepa kumpa msaada, baadaye alipokelewa.
Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mount Meru, Omar Chande, alithibitisha kumpokea mgonjwa huyo na kueleza kuwa, kwa sasa wanachokifanya na kumpatia tiba mchanganyiko.
“Ni kweli tulimpokea mgonjwa huyo akitokea Patandi Meru, lakini tunaendelea kumpatia tiba mchanganyiko, ikiwemo ya malaria, ambayo alikutwa nayo pamoja na dengue maana hadi sasa hii homa haina tiba maalumu,” alisema na kuongeza kuwa hali yake kwa sasa inaendelea vizuri.
Dengue tishio zaidi Dar
Juzi, serikali iliziagiza Halmashauri za Manispaa za mkoa wa Dar es Salaam, kusimamia mara moja upuliziaji dawa katika maeneo yenye mkusanyiko ili kukabiliana na ugonjwa wa homa ya dengue.
Imeziagiza Manispaa za Ilala, Temeke na Kinondoni, kutenga fedha za dharura kwa ajili ya kupambana na ugonjwa huo.
Aidha, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), imetakiwa kuandaa utaratibu wa kupulizia dawa mabasi yote yaendayo mikoani, meli na treni ili kuepuka kusambaa kwa ugonjwa huo.
Agizo hilo lilitolewa na Mkuu wa Mkoa, Meck Sadiki, ambapo pia alieleza hatua mbalimbali zinazochukuliwa na serikali katika kudhibiti ugonjwa huo.
Ugonjwa huo ni mpya hapa nchini na ulianza mwishoni mwa Januari, mwaka huu na tangu ulipothibitika kuwa upo Dar es Salaam, karibu watu 523 walipimwa.
Kati ya watu hao, 414 walithibitika wana dengue ambapo Kinondoni walikuwa 342, Temeke 20 na Ilala 52.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru