Tuesday 13 May 2014

Lissu avurugwa


  • Alidanganya tena Bunge kuhusu Muungano
  • Wabunge wamlipua mapenzi yake kwa Z’bar

CHARLES MGANGA NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
HALI ya Msemaji wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu, jana ilikuwa tete baada ya wabunge kuamua kumtolea uvivu kutokana na kauli zake za uwongo zilizodaiwa kuwa zina lengo la kupotosha umma.
Huku wakionyesha mifano, wabunge wengi waliosimama walimshambulia Lissu kwa kupotosha umma kuhusu masuala mbalimbali ya Muungano huku mengi yakidaiwa kuwa hayana tija wala ushahidi wa kutosha.
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati wa kujadili Hotuba ya Makadirio na Matumizi ya Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), awali, Lissu, aliwasilisha taarifa ya Kambi ya Upinzani.
Naibu wa Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba, ndiye aliyekuwa mwiba kwa Lissu, ambapo alisema mbunge huyo amezoea kusema mambo ambayo hayafahamu wala kuwa na uhakika nayo.
Mwigulu, ambaye alikuwa akijibu baadhi ya hoja zilizohusu wizara yake, alisema fedha za misaada kwa kawaida wafadhili hutoa maelekezo ambapo katika hilo, kiasi cha usawa wa asilimia 4.5 hutengwa kabla ya kufanya mgawo husika.
“Naomba tu kwanza niweke kumbukumbu sawa. Fedha wanazopaswa kupata Zanzibar, zimekuwa zikitolewa kwa miaka yote mfululizo kama kawaida.
“Unajua kama mambo huyajui, ni vyema ukauliza. Hata ndugu zangu wa Zanzibar, ni kwa nini msiwaulize viongozi wenu. Bahati nzuri kuna kitengo kinachohusu masuala ya fedha, kuliko kufanya mambo yasiyo na ushahidi.
“Kwa kwaida, fedha za wafadhili ambazo zitatolewa ndivyo mgawo utakavyofanywa. Sasa kama hii iliyoelezwa kwenye hotuba ya kambi ya upinzani kwamba zilitakiwa kiasi cha sh. Bilioni 32. Tulizozipata, tumetafuta uwiano wa 4.5, kiasi kilichobaki tutapeleka Zanzibar,” alisema Mwigulu ambaye pia ni Mbunge wa Iramba Magharibi (CCM).
Alishauri kuwepo kwa utaratibu wa kutoa takwimu zinazohusu fedha ili kuwezesha akina Lissu kuelewa kabla ya kuzungumza ndani ya bunge.
Pia, aliwahadharisha wabunge wa Zanzibar kuwa, mambo yaliyozungumzwa na Lissu katika hotuba yake, hayaonyeshi kuwa ana mapenzi ya dhati kwa wananchi wa visiwa hivyo.
“Unajua mtu huyo baada ya kuona chuki aliyoipandikiza Tanzania Bara imekosa mashiko, ameamua kuhamia Zanzibar. Mkivurugana yeye atabaki Singida.
Akinukuu maneno ya Lissu aliyoyatoa mwaka jana kuwa kero za Muungano si mali binafsi ya wabunge, alisema hata watanzania wanakerwa na ubaguzi unaofanywa na Wazanzibari, jambo ambalo ni kinyume cha anayoyasema sasa.
Katika kuonyesha Lissu ni kigeugeu, Mwigulu alisema aliwahi kusema kwamba, Wazanzibari walikuwa wakipendelewa kinyume na jinsi hotuba yake inavyoeleza.
“Yaani wakati mwingine napata shida kuamini kama Lissu ametokea Singida kule ninakotoka mie,” alisema.
Awali, wakichangia hoja hiyo, Mohamed Amour Chombo, alimshangaa Lissu kuwa na mapenzi na watu wa Zanzibar huku awali alikuwa akiwapinga na kuwatolea maneno ya karaha na yenye kukera.
Chiombo, alisema muungano wa sasa baina ya CHADEMA na CUF ni sawa na kuchepuka na kwamba, CUF wanapaswa kuwa macho na Lissu.
“Ndugu zangu acheni mchepuko, rudini njia kuu, hawa wanawapenda leo wana nia yao si bure wenzenu ni sisi,’’ alisema Chombo.
Chombo alisema hotuba ya Lissu ni ya uchochezi na kuwataka watanzani kutokubali kuingizwa katika uchochezi.
“Wewe unaposema muungano hauna maana ujue fedha za uwanja wa ndege zimetokana na nini, acheni michepuko rudini njia kuu.
“Kuna baadhi ya watu wakishapata wimbo Fulani, basi kila wakati atauimba huo huo wakati akienda kula, akienda wapi, sasa ni sawa na Lissu amepata wimbo wa muungano ni huo huo,’’ alisema.
Aidha, kwa upande wake Steven Masele, aliweka rekodi sawa aliposema Wizara ya Mambo ya Nje imewahi kuwa na Waziri kutoka upande wa Zanzibar.
Masele, alisema hayo baada ya kuzuka hoja kwamba Muungano uliopo una upendeleo kwa viongozi wanaotoka Tanzania Bara.
“Jamani niwakumbushe tu kwamba Ahmed Hassan Diria (Marehemu), aliwahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,” alifafanua Masele.
Wakati akijibu hoja za baadhi ya wabunge waliochangia ofisi ya Makamu wa Rais, Waziri Samia Suluhu Hassan, aliahidi kushughulikia changamoto hizo na kuzipatia ufumbuzi wenye tija.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru