Tuesday 20 May 2014

‘Nyumba za Chamwino ni za wasaidizi wa Rais’


SERIKALI imesema haiwezi kukabidhi nyumba zilizopo katika kijiji cha Chamwino kwa Halmashauri ya Chamwino kwa kuwa nyumba hizo ni kwa ajili ya watumishi ambao wamekuwa wakiongozana na Rais anapokwenda Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Sophia Simba alisema hayo bungeni jana mjini hapa alipokuwa akijibu swali la Hezekiah Chibulunje (Chilonwa-CCM) aliyetaka kujua kwanini nyumba hizo zisikabidhiwe kwa Halmashauri ya Chamwino.
Waziri Simba alisema nyumba za watumishi zilizopo Ikulu Ndogo ya Chamwino zimedhamiriwa kuwa makazi ya muda ya watumishi wasaidizi na washauri wa Rais wakati wanapokuwa Chamwino na kwamba  hutumika kwa kutegemea ratiba ya Rais anapokuwa Dodoma .
Aliongeza kuwa  kuchakaa kwa nyumba hizo si kwa sababu ya kutokaliwa, isipokuwa  zimejengwa muda mrefu uliopita.
Alisema kutokana na kukosekana kwa fedha, serikali imeshindwa  kuzifanyia ukarabati mkubwa, lakini itaendelea kuzikarabati kwa awamu .
Alisema katika mwaka wa fedha wa 2014/2015, serikali imetenga sh. bilioni mbili kwa ajili ya ukarabati wa nyumba hizo pamoja na mazingira yake.
Waziri Simba alisema serikali inatambua kuwa Chamwino ni wilaya mpya yenye changamoto nyingi, likiwemo tatizo la ukosefu wa nyumba za kuishi watumishi na kuwalazimisha baadhi yao kuishi Dodoma Mjini.
Alisema serikali imewasiliana na uongozi wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na kuliomba lijenge nyumba za kupangisha Chamwino.
Alisema shirika hilo limekubali  na kwa sasa halmashauri imeombwa kutenga viwanja na kuwasilisha rasmi maombi ya kujengwa kwa nyumba hizo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru