Friday 9 May 2014

Mjumbe Wazazi Mara adaiwa kudanganya

Na Latifa Ganzel, Morogoro
JUMUIA ya Wazazi mkoa wa Morogoro imemtaka mjumbe wa baraza kuu la Wazazi Taifa mkoa wa Mara, kutowaingiza katika migogoro na viongozi wa kitaifa kwa kuandika habari za uongo katika vyombo vya habari.
Katibu wa Wazazi mkoa wa Morogoro, Abdalla Shaweji, alisema hayo jana alipozungumza na waandishi wa habari mkoani hapa, kufuatia taarifa zilizoandikwa katika gazeti moja la kila siku zikimtuhumu Mwenyekiti wa Wazazi Taifa, Abdallah Bulembo, kuwa alihoji uhalali wa mjumbe huyo kuwepo katika kikao cha Baraza la Mkoa wa Morogoro lililofanyika hivi karibuni.
Shaweji, alisema Jeremia alidai katika gazeti hilo kuwa yeye ni mjumbe halali wa baraza hilo wakati si sahihi na kwamba, hakuwepo siku hiyo.
“Tunamshangaa sana Jeremia kusema kuwa yeye ni mjumbe halali wa baraza la mkoa wa Morogoro wakati yeye anatoka mkoa wa Mara, lakini pia siku ya baraza hakuwepo,’’ alisema.
Alisema Jeremia alinukuliwa katika gazeti hilo kuwa Mwenykiti Bulembo alifungua kikao hicho na kufunga wakati si sahihi na kwamba, Bulembo alifungua baraza hilo lililofungwa na katibu wa mkoa wa Morogoro, Rojas Romuli.
Alisema anashangaa kuona habari hizo zimeandikwa na mwandishi ambaye hakuwepo katika kikao hicho na kwamba, aliyekuwepo ambaye ni Ramadhani Libenanga, alidai hajui chochote juu ya habari hiyo.
Alisema mkoa wa Morogoro hawana tatizo na Mwenyekiti Bulembo na kwamba, asiwahusishe na kuwaingiza katika migogoro isiyowahusu.
Alimtaka Jeramia kuliomba radhi baraza la mkoa wa Morogoro kwa kutoa taarifa za uongo, vinginevyo watamchukulia hatua ikiwa ni pamoja na kukiandikia barua Chama na Jumuiya hiyo kulalamikia suala hilo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti Wazazi Mkoa wa Morogoro, Mecktridic Mdaku, alisema amesikitishwa na taarifa hizo ambazo si sahihi na kusema kuwa wanayo mikanda ya video waliyochukua siku hiyo na kwamba, wamehifadhi kama vielelezo vya tukio hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru