Tuesday 20 May 2014

Vigogo CHADEMA waipinga UKAWA



  • Wasema ni kikundi cha wahuni, wasaka maslahi
  • Nape ataka wasibembelezwe kurejea bungeni
  • Mgeja amvurumishia makombora mazito Dk. Slaa

NA WILLIAM SHECHAMBO
MAMBO si shwari ndani ya CHADEMA kutokana na baadhi ya viongozi wake kulishukia kundi la Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA) kwa kuendesha siasa chafu.
Viongozi hao wa CHADEMA wakiwemo Wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho, wamesema wanachokifanya UKAWA ni uhuni wa kisiasa.
Wajumbe hao kutoka mikoa ya Tanga, Dar es Salaam na Pwani, wamesema wamefikia hatua hiyo kutokana na malalamiko na manung'uniko ya wanachama wa chama hicho kuhusu udhaifu mkubwa wa viongozi wa ngazi za juu chini ya mwavuli wa UKAWA.
Wakizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana wakati wakitoa tamko hilo na mustakabali CHADEMA na UKAWA, walisema umoja huo umeundwa kihuni na watu wachache kwa madhumuni ya kupata maslahi.
Walieleza kusikitishwa na tabia ya viongozi na wabunge wa CHADEMA, kusahau majukumu yaliyowapeleka bungeni, ambayo ni kuandika katiba mpya yenye kuzingatia maslahi ya Watanzania na badala yake kuanzisha siasa chafu na kushiriki kwenye vikundi vya kihuni.
"Kwa namna ambavyo tumepambana kwa miaka mingi kudai na kuishinikiza serikali kuridhia uandikaji wa katiba mpya, ni limbukeni pekee anayeweza kususia fursa ya uandishi huo, tena kupitia chombo huru (Bunge la Katiba) kwa sababu ya mgongano wa kimaslahi.
"Tunaomba ifahamike kwamba, hakujawahi kukaa kikao chochote halali kilichoazimia na kuwaagiza wajumbe wanaotokana na chama chetu wasimamie katiba yenye serikali tatu, hayo ni maamuzi ya wachache," walisema wajumbe hao.
Kwa mujibu wa mwakilishi wao, Joseph Patrick, ambaye ni Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Chadema Taifa, alisema UKAWA ni unafiki wa kisiasa, ambao umebuniwa ili viongozi wagawane vyeo.
Alisema hakuna sababu yoyote yenye mantiki iliyopo katika uundwaji wa umoja huo na ndio sababu hauna rejea wala hati za makubaliano.
Alisema UKAWA ilianzishwa bila kuwashirikisha wanachama wa chama hicho, hivyo kitendo cha Mwenyekiti wao, Freeman Mbowe, kuamua bila kuwepo kwa vikao halali, kumeondoa umaana wa wajumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu kwenye utoaji maamuzi ndani ya chama.
"Kiongozi wetu ameonyesha dharau ya hali ya juu, hivyo ninapenda kuwaambia watanzania kuwa, sisi baadhi ya wajumbe wa Baraza Kuu na mkutano mkuu, hatuungi mkono upuuzi wowote wenye lengo la kusimamia ugawanaji wa vyeo na madaraka, watu wa namna hii tunawaita walafi wa madaraka," alisema kiongozi huyo.

Nape: UKAWA wasibembelezwe  
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye, alisema  UKAWA hawapaswi kubembelezwa kurejea bungeni.
Alisema CCM haikwenda Tabora kushughulika na UKAWA na kwamba ziara ya Chama mkoani humo ilikuwa ya kushughulikia matatizo ya wananchi.
Nape alisema wengi wa viongozi wa UKAWA wanasumbuliwa na njaa kwa hiyo hawana hoja.

Slaa acha siasa za kitoto- Mgeja
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amemtaka Katibu Mkuu wa (CHADEMA), Dk. Wilbroad Slaa kuacha siasa za kitoto.
Amesema kitendo cha Dk. Slaa kumsakama Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana, na kumtaka kuacha kufanya vikao na watendaji na watumishi wa serikali, ni ishara ya kiongozi huyo kutofahamu kuhusu utendaji wa serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Mgeja alisema CCM ndiyo yenye serikali hivyo, ziara za Kinana na timu yake ni kuangalia utekelezaji wa kazi za serikali na imo kwenye Ilani ya CCM.
Mgeja alisema Dk. Slaa anamuonea wivu Kinana kutokana na utendaji kazi bora na wenye mafanikio unaofanywa na serikali ya CCM.
CCM kuisimamia serikali yake sio dhambi, kwani ni sawa na mwenye shamba kukagua eneo lake na mfugaji kukagua mifugo. Huyu anazeeka vibaya mno. Kinana anafanya kazi za wananchi, yeye (Slaa) kazi ni kuzunguka kukusanya posho za UKAWA, sasa atulie aonyeshwe jinsi watendaji wa vyama wanavyotakiwa kufanya kazi,î alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru