Wednesday 14 May 2014

TANESCO yazindua mradi mpya


NA RABIA BAKARI
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO), limezindua mradi wa kukarabati vituo vinavyozalisha umeme ili kuongeza kiwango cha uzalishaji wa nishati hiyo.
Mradi huo unaotekelezwa kwa ushirikiano na Serikali ya Norway, umegawanywa katika utekelezaji wa awamu ya pili, ya kwanza ni ukarabati wa dharura na pili  ukarabati mkubwa utakaochukua muda mrefu.
Akizungumza katika mahojiano na waandishi wahabari, baada ya ufunguzi wa mradi huo, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO,  Injinia Boniface Njombe, alivitaja vituo vitakavyofanyiwa ukarabati kuwa ni pamoja na Kidatu, Mtera, Kihansi, Nyumba ya Mungu na Mto Pangani.
Alisema vituo hivyo vilijengwa muda mrefu na vinafanya kazi mfululizo.
Hata hivyo, alisema baada ya kulibaini hilo, walifikiria mbinu mpya ya kuviboresha.
“Lengo ni kuleta ufanisi, kuongeza ufanyaji kazi na kuvifanya vituo vidumu kwa muda mrefu, tuliamua kuanza kutafuta wadau wa kutusaidia katikahili,” alisema.
Alisema serikali ya Norway imetoa zaidi ya sh.bilioni 1.8, huku Tanzania ikitoa fedha mara tatu ya hiyo, kwa ajili ya ukarabati wa dharura, huku ukarabati mkubwa ukiendelea kufanyiwa tathmini kujua gharama halisi.
Injinia huyo alisema ingawa kuna makandarasi wawili walioteuliwa kufanya kazi hiyo, wanashirikiana na Mamlaka ya Usimamizi wa Maji na Nishati kutoka Norway (NVE).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru