Wednesday 14 May 2014

Aua shemeji, kisa mbwa kula mayai


NA SAMSON CHACHA, TARIME
MKAZI wa Kijiji cha Nyamwaga wilayani hapa mkoani Mara, Mbusiro Muyuyi, ameuawa kwa kukatwakatwa kwa panga kichwani na shemeji yake.
Mauaji hayo yaliyowashitua wengi wilayani hapa, chanzo chake ni mbwa wa mtuhumiwa, Mwita Muyuyi (17), kula mayai ya kuku wa marehemu.
Habari za kuaminika zimesema kuwa, Mbusiro (45), alimtuhumu shemeji yake kuwa, mbwa wake amekula mayai ya kuku, hali iliyoibua mzozo mkubwa baina yao.
Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Tarime/ Rorya, Justus Kamugisha, alisema tukio hilo lilitokea juzi asubuhi katika kitongoji cha Ntarachagine.
Alisema wakati mzozo huo ukiendelea, Muyuyi alikuwa ameshika panga na ghafla alianza kumshambulia mke wa kaka yake sehemu mbalimbali za mwili wake.
Kamanda Kamugisha alisema baada ya tukio hilo, Mbusiro alikimbizwa hospitali kwa matibabu, lakini akiwa kwenye zahanati ya Nyarero, hali yake ilizidi kuwa mbaya na kufariki dunia.
Tayari mtuhumiwa anashikiliwa na polisi kwa uchunguzi zaidi kabla ya kupandishwa kizimbani kujibu tuhuma za mauaji zinazomkabili.
Kamanda Kamugisha alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuacha tabia za kujichukulia sheria mkononi na badala yake wafikishe migogoro kwenye vyombo vya ulinzi na usalama kwa hatua zaidi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru