Wednesday 14 May 2014

CHADEMA yazidi kupasuka Arusha


NA SHAABAN MDOE, ARUSHA
WAFUASI na wanachama wa CHADEMA mkoani hapa, wameendelea kukikimbia chama hicho na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Hiyo inatokana na zaidi ya wanachama 100 wa CHADEMA wilaya Arusha, akiwemo Mjumbe wa Kamati ya Utendaji wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Ruaichi Kivuyo, naye kujiunga na CCM.
Mbali na Kivuyo, vigogo wengine waliokihama CHADEMA ni Mwenyekiti wa Kata ya Unga Ltd, Swalehe Ally na Katibu Mwenezi wake, Obuyah Juma.
Akizungumza juzi katika mkutano wa hadhara uliofanyika eneo la Esso, uliokuwa na lengo la kukagua utekelezaji wa Ilani ya CCM, Kivuyo, alisema amelazimika kuchukua uamuzi huo baada ya kujiridhisha kuwa CHADEMA imepoteza mwelekeo.
Alisema uhakika wa chama hicho kupoteza dira na mwelekeo aliupata baada ya Wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba wanaotokana na UKAWA, kususia vikao hivyo.
Alisema kikundi hicho cha UKAWA tafsiri yake ni usaliti, kwa kuwa wao ndiyo waliyoiomba katiba mpya, hawakupaswa kususia majadiliano, bali kutetea hoja zao ndani ya bunge hilo hata kama wako wachache, wananchi na wanachama wangeona wamezidiwa, lakini si kutoka nje.
Naye aliyekuwa Mwenyekiti wa CHADEMA Kata ya Unga Ltd, Swalehe, alisema hawezi kuendelea kuvumilia maumivu na laana kutoka kwa wananchi, kutokana na vurugu zinazofanywa na Mbunge wa Arusha Mjini, Godbles Lema.
Alisema wananchi kwa sasa wamechoshwa na vurugu hizo, kwakuwa hazina msingi wowote wa kimaendeleo bali unawafanya vijana kukosa uzalendo kwa taifa lao.
Aidha, alisema amechoshwa na tabia ya uongozi wa chama hicho kung’ang’ania ruzuku ya chama taifani bila kufika mikoani, wilayani na mpaka katika kata, jambo ambalo linawasababishia hasara kubwa kwa kulazimika kutumia fedha zao binafsi kufanya shughuli za chama.
“Hiki chama gani kisicho na mizizi wala shina bali matawi tuu, sasa kitasimamaje, haya, sisi mizizi na mashina tunajiondoa. Tumechoka na ubabaishaji wa viongozi wa juu,” alisema Swalehe.
Mwenyekiti wa UVCCM Wilaya ya Arusha, Martin Munis, aliwataka wanachama hao wapya kusahau machungu yote ya CHADEMA kwani wamekwenda mahali sahihi.
Aliwataka kutangaza msimamo wa CCM katika kuunga mkono muundo wa serikali mbili kama mtihani wao wa kwanza, lakini pia, kuwahamasisha vijana kujiunga katika vikundi vya ujasiriamali ili waweze kukopesheka na kujiinua kimaisha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru