Thursday 29 May 2014

Hakimu, karani kortini kwa rushwa ya 50,000/-


NA SYLVIA SEBASTIAN
HAKIMU wa Mahakama ya Mwanzo Buguruni, Dar es Salaam, Grace Kivelege na karani wake, wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Wilaya Ilala, kujibu mashitaka ya kuomba na kupokea rushwa ya sh. 50,000.
Hakimu Grace na Karani Rose Kuhima, walifikishwa mahakamani hapo jana na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Wakili wa TAKUKURU, Devota Mihayo, aliwasomea washitakiwa hao mashitaka mawili ya kuomba na kupokea rushwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Juma Hassani.
Devota alidai washitakiwa hao walitenda makosa hayo Mei 7, mwaka huu, katika Mahakama ya Mwanzo Buguruni,  wilayani Ilala.
Katika shitaka la kwanza linalomkabili Hakimu Grace, anadaiwa Mei 5, mwaka huu, mahakamani hapo, akiwa mwajiriwa, alimshawishi Clementina Guruma, kumpatia sh. 50,000, kama kichocheo cha kutoa rushwa ili aweze kumsaidia kesi iliyokuwa mbele yake.
Shitaka la pili, Hakimu Grace na karani wake, wanadaiwa Mei 7, mwaka huu, katika mahakama hiyo, walipokea rushwa hiyo kutoka kwa Clementina.
Washitakiwa walikana mashitaka hayo, ambapo Devota alidai upelelezi umekamilika na kuomba tarehe ya usikilizwaji wa awali. Pia Devota alidai hana pingamizi juu ya dhamana kwa washitakiwa.
Washitakiwa hao waliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili waaminifu, watakaotia saini bondi ya sh. milioni mbili. Kesi hiyo iliahirishwa hadi Juni 11, mwaka huu, kwa usikilizwaji wa awali.
Wakati huo huo, Ally Yahya (24), alifikishwa Mahakama ya Mwanzo Kariakoo, kujibu shitaka la wizi wa vifaa vya gari vyenye thamani ya sh. 100,000.
Mbele ya Hakimu Mfawidhi, Matrona Luanda, Karani Blanka Shao, alidai Juni 23, mwaka huu, saa mbili asubuhi, maeneo ya Faya, mshitakiwa aliiba futo mbili za gari zenye namba ya usajiri T. 701CVF Toyota Rauni zenye thamani ya sh. 100,000, mali ya Vicent Mnyanyika.
Mshitakiwa alikana shitaka hilo na alirudishwa rumande hadi Juni 10,mwaka huu kutokana na kutotimiza masharti ya dhamana.
Hakimu Matrona aliyataja masharti hayo kuwa ni wadhamini wawili watakaotia saini bondi ya sh. 200,000.     

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru