Tuesday 13 May 2014

Wauguzi wanne hoi kwa Dengue



  • Wengine wapoteza maisha, 400 wana virusi

Na waandishi wetu
SERIKALI imesema watu wanne wamepoteza maisha huku wengine 400 wakibainika kuwa na virusi vya ugonjwa wa homa ya Dengue.
Ugonjwa huo ambao umeanza kuenea katika maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam, umekuwa tishio hadi kwa madaktari na wauguzi, ambapo hali si shwari katika Hospitali ya Temeke.
Tayari Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Akili, Gillbert Bubelwa (36), amepoteza maisha huku wauguzi wanne wa hospitali hiyo wakilazwa kwa matibabu baada ya kushambuliwa na virusi vya ugonjwa huo.
Akizungumza wakati akitoa taarifa kwa Mbunge wa Temeke, Abbas Mtevu, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Temeke, Amaani Malima, alisema mpaka sasa wamempoteza Dk. Bubelwa na Muuguzi wa Kitengo cha Akina mama, Hamida Likoti (37).
Alisema tangu kulipuka kwa ugonjwa huo, wamepokea wagonjwa 36, kati yao, 16 wamegundulika kuwa na virusi vya Dengue huku wengine wakiwa na dalili.
Naye Daktari Kiongozi wa Hospitali ya Amana, Andrew Method, alisema katika kipindi cha mwezi Februari hadi Mei, mwaka huu, wamepokea wagonjwa 110 na tisa kati yao wakigundulika kuwa na ugonjwa huo.
Alisema wagonjwa sita walitibiwa na kuruhusiwa na 95 wenye dalili za ugonjwa huo wanaendelea na matibabu.
Hata hivyo, alisema changamoto kubwa ni uhaba wa vipimo na ameiomba serikali kuuchukulia ugonjwa huo kwa uzito unaostahili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Charles Pallangyo, alisema serikali imepanga kukabiliana na ugonjwa huo kwa kutoa mafunzo kwa watumishi wa afya, ikiwemo madaktari na wataalamu wa maabara.
Alisema kwa kuanzia, mafunzo yametolewa kwa Hospitali za Mkoa wa Dar es Salaam na yataendelea kutolewa nchini kote.
“Wizara imetoa maelekezo kwa Waganga Wakuu wa Mikoa na Wilaya kutoa taarifa za watu walioathiriwa na virusi vya ugonjwa huo kila wiki.
“Tumeanzisha vituo maalumu vya ufuatiliaji katika hospitali za Muhimbili, Mwananyamala, Amana na Temeke,” alisema.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru