Wednesday 28 May 2014

Profesa Tibaijuka akabidhi hatimiliki za kimila Mvomero


NA REHEMA ISANGO
SERIKALI imeanza kwa vitendo kutatua migogoro ya kudumu ya ardhi na upimaji wa kila kipande, baada ya kutoa hatimiliki za kimila katika kijiji cha Lekenge, wilayani Mvomero mkoani Morogoro.
Utatuzi huo ulianza juzi baada ya  Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka, kukabidhi hati hizo kwa wananchi wa kijiji hicho.
Akizungumza katika hafla ya kukabidhi hati hizo, Profesa Tibaijuka alisema hatimiliki za kimila zina faida kubwa, ambapo mbali ya kutatua migogoro, zinasaidia katika kupata mikopo kwenye taasisi za fedha.
Akizungumzia ufugaji, alisema kufuga ni haki na kazi  na ni ruksa kwa kila mtu kufanya hivyo, lakini kinachotakiwa ni kufuga kwa kufuata utaratibu, ikiwemo kufuata ufugaji wa kisasa.
Alisema  migogoro inayoibuka mara kwa mara kati ya wafugaji na wakulima, kwa kiasi kikubwa inatokana na aina ya ufugaji, ambapo wafugaji wengi wanaendelea kutumia mbinu za kizamani za ufugaji wa kuhamahama.
Profesa Tibaijuka alisema katika siku zijazo, wafugaji watatengewa maeneo kwa kila mfugaji, hivyo wanapaswa kujiandaa kujiunga kwenye vikundi vya ushirika ili waweze kwenda na wakati.
Alisema kwa sasa serikali inafanya jitihada za kuwatafutia wafugaji maeneo kwenye ranchi za taifa na mapori ya akiba, ambayo yatawekewa uzio ili  mifugo isitoke na kwenda kwenye mashamba ya wakulima.
Kuhusu hatimiliki za kimila, Profesa Tibaijuka aliwaasa waliopimiwa mashamba kuwa,   wanapaswa kujenga barabara ili maeneo yao yaweze kufikika na wahusika waweke mipaka kwa kupanda miti ya kijadi.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dk. Selassie Mayunga, aliwaahidi wananchi hao kutekeleza ahadi yake ya kuwachimbia kisima kimoja.
Alisema kutokana na kukamilika kwa upimaji huo wa ardhi,  migogoro ya wakulima na wafugaji itamalizika kwa kila jamii kugawiwa ardhi na kila kipande cha ardhi kuwa na matumizi yaliyoainishwa kwenye ramani ya kijiji.
Katika  risala yao, wananchi wa Lukenge walisema wamepokea mpango huo kwa furaha kubwa kwa kuwa utasaidia kumaliza migogoro ya ardhi, iliyokuwa ikijitokeza mara kwa mara.
Katika mgogoro wa wakulima na wafugaji mwaka jana, baadhi ya wananchi wa kijiji hicho, walikimbia nyumba zao na kwenda kupata hifadhi kwenye Kiwanda cha Sukari cha Mtibwa.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru