Thursday 8 May 2014

Walimu wacharuka kudai mishahara


NA PETER KATULANDA, MWANZA
WALIMU wapya wapatao 100 kati ya 164, kutoka katika shule za msingi na sekondari wilayani Nyamagana, wameandamana kudai mshahara wa mwezi uliopita na nauli.
Waliandamana jana mchana kutoka katika shule mbalimbali hadi katika Ofisi za Jiji la Mwanza, huku wakitishia kulala katika jengo hilo iwapo hawatalipwa stahiki zao ambazo ni zaidi ya sh milioni 80.
Akizungumza kwa niaba ya wenzake, Mwalimu wa Sekondari ya Fumagila iliyopo Igoma, Ludovick Luis, alisema hawajalipwa mshahara wa mwezi Aprili hivyo, kuwafanya waishi kwa shida ikizingatiwa kuwa ndiyo wanaanza maisha.
ìLicha ya mshahara, pia tunadai nauli zetu tulizotumia kusafiri kutoka kwetu kuja kwenye vituo vya kazi ,vinginevyo kuandamana haitoshi, tutalala hapa hadi kieleweke maana tunaishi kwa shida ikizingatiwa ndiyo tunaanza kazi, tuna mahitaji mengi,î alisema.
Walimu hao walidai wenzao 43 kati ya 164 waliopata ajira hizo mpya wilayani Nyamagana, wamelipwa mshahara na stahiki zao.
Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza, Danford Kamenya, alisema walimu 43 kati ya 164 wamelipwa, 101 majina yao yanaendelea kuhakikiwa wizarani, wanne wamepangiwa vituo vingine nje ya jiji hilo na sita vyeti vyao vina utata.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru