Thursday 8 May 2014

CAG aibua mapya



  • Watumishi hewa wazidi kuikamua serikali
  • Vyama vya siasa vinne havina akaunti benki
  • Misamaha ya kodi, wanyamapori vyaguswa 

NA CHARLES MGANGA, DODOMA
MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, amekabidhi bungeni ripoti ya mapato na matumizi ya serikali yanayoishia Juni, mwaka 2013 na kubaini changamoto kadhaa.

Akizungumzia taarifa yake aliyoitoa kwa waandishi wa habari mjinji hapa jana, Utouh alisema kumekuwa na mafanikio yanayoonekana ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa utendaji wa serikali katika kusimamia makusanyo ya mapato na matumizi ya rasilimali umma ikilinganishwa na miaka iliyopita.
Utouh, alisema kuimarika huko kumetokana na ofisi yake kutoa hati za ukaguzi, kati ya hizo, 816 sawa na asilimia 85, ziliridhisha.
Alisema, idadi ya hati zenye shaka ni 131 ambazo ni sawa na asilimia 13.6, hati zisizoridhisha ni nane sawa na asilimia 0.8 na hati mbaya zilikuwa sita, sawa na asilimia 0.6.
Aidha, alisema eneo la deni la taifa na misamaha ya kodi, limeonekana kuwa na changamoto, licha ya mafanikio yaliyopatikana.
Hata hivyo, alisema kazi ya ukaguzi wa deni la taifa na misamaha ya kodi, bado inaendelea.
Pamoja na kazi hiyo kuendelea, Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu amegundua baadhi ya masuala kadhaa, ikiwa ni hali halisi ya deni la taifa ambalo lilifikia sh. trilioni 21.20, ongezeko la sh. trilioni 4.23 sawa na asilimia 25 ikilinganishwa na sh. trilioni 16.98 kwa mwaka 2011/2012.
Kwa mujibu wa CAG, deni halisi la ndani lilifikia sh. trilioni 5.78 kwa mwaka ulioishia Juni 2013, ikiwa ni ongezeko la sh. Trilioni 1.23 sawa na asilimia 27 kutoka kiasi cha sh. trilioni 4.55 kwa mwaka 2011/2012.
Alisema, ongezeko hilo limesababishwa na mikopo kutoka katika benki mbalimbali na wafadhili tofauti kwa ajili ya kusaidia miradi mikubwa ya maendeleo kama vile uboreshaji wa miundombinu katika nyanja za usafirishaji, maji safi, mkongo wa mawasiliano ya taifa na bomba la gesi.
Alipendekeza pamoja na deni la taifa kuongezeka, uchumi wa nchi nao umekuwa na kuimarika kutokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Alisema serikali kupitia Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imekuwa ikitoa misamaha ya kodi kwa mujibu wa kanuni na sheria kwa walengwa ikiwa na dhamira ya kukuza biashara.
Kuhusu ukaguzi wake aliofanya katika vyama vya siasa, Utouh amegundua upungufu kadhaa.
Miongoni mwa upungufu huo ni vyama vinne kutokuwa na akaunti, hivyo hesabu zake kukosa ushahidi wa kutosha.
CAG alivitaja vyama hivyo visivyo na akaunti kuwa ni pamoja na UMD, NLD, NRA na ADC.
Alisema, vyama vya siasa 11 kati ya 21 vyenye usajili wa kudumu, havikuwasilisha taarifa za hesabu za Juni mwaka 2013 kwa mujibu wa kifungu cha 14 (i)(b)(i) cha sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.
Alisema hata taarifa zilizowasilishwa, hazikufuata misingi ya uhasibu na mfumo wa utoaji taarifa za fedha za kimataifa.
Alisema, mali za vyama saba vilivyokaguliwa, havionyeshi mali za kudumu na zile za muda mfupi inazozimiliki kinyume cha kifungu cha sheria ya kifungu cha 14 (1) cha sheria ya vyama vya siasa namba 5 ya mwaka 1992.

MISHAHARA HEWA

Katika eneo hili, CAG alisema katika ukaguzi wake aligundua kuwepo kwa watumishi hewa kuendelea kulipwa mishahara.
Watumishi hewa hao ni wale waliofariki dunia, kustaafu na walioacha kazi, ambapo mishahara yao imeendelea kupelekwa kwenye akaunti zao.
“Katika eneo hili, hata yale makato ya mifuko ya hifadhi za jamii kama NSSF, bima ya afya, yamekuwa yakifanyika,” alisema.
Alisema, hali hiyo imefanya serikali kupoteza kiasi cha sh. bilioni 1.62 na makato yake ni sh. milioni 497.
Alisema, hali hii bado imeendelea licha ya serikali kuwekeza katika mfumo wa LAWSON kama njia mojawapo ya kudhibiti hali hiyo.
Alisema kuna umuhimu kwa serikali kudai fedha zilizolipwa isivyo halali kutoka mifuko ya hifadhi ya jamii, mamlaka ya mapato (TRA) na benki.
“Kwa mtu mmoja mmoja ni vigumu fedha hizo kurejeshwa, lakini hizi zilizokwenda maeneo hayo, ni vyema serikali ikazidai,” alisema Utouh.

UWINDAJI NA WANYAMAPORI

Katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2013, ripoti ya eneo hili unaonyesha kuwa doria hazikufuatiliwa na kufanyiwa tathimini ipasavyo.
Udhaifu katika usimamiaji wa sheria zinazotumika kutoa adhabu kwa wahalifu wanaohusika na vitendo viovu vya kuangamiza wanyamapori, ni tatizo lililobainika.
CAG aligundua Wizara kushindwa kufanya tathimini ya kina kwa kampuni za uwindaji kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi mwaka 2012.
Jambo jingine ni kutokuwa na utaratibu sahihi wa kusimamia ukusanyaji wa mapato. Ukaguzi ulibaini kampuni 36 hazijalipa ushuru kwa utalii wa picha na kuisababishia serikali hasara ya mapato ya sh. Bilioni 2.7.
Alisema hasara hii ilitokana na kutokuwepo kwa usimamizi mzuri katika kusimamia utalii wa picha.
Akizungumza baada ya CAG, Mwenyekiti wa kamati ya serikali (PAC), Zitto Kabwe alipongeza kwa ripoti hiyo kuwasilishwa kwa wakati.
“Kwa kawaida CAG amekuwa akiwalisha ripoti ya mapato na matumizi bungeni Aprili, lakini imeshindikana kufanya hivyo kutokana na vikao vya bunge la katiba kuendelea wakati huo,” alisema Zitto.
Alisema, changamoto zilizoonekana kamati itazifanyia kazi ili mwaka ujao wa fedha, zipatiwe ufumbuzi.
Naye Mwenyekiti wa kamati ya Hesabu za serikali za mitaa (LAC), Rajabu Mbaruku, alisema suala la mishahara hewa ni changamoto kubwa inayohitaji utatuzi wa haraka.
“Kupoteza kiasi cha sh. bilioni 1.6 ni kiasi kikubwa cha fedha. Hizi ni fedha zinazolipwa na watu bila huruma, hili ni jambo la kufanyiwa kazi haraka,” alishauri Mbaruku.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru