Thursday 15 May 2014

Walimu Uyui walia na Dk. Kawambwa


WALIMU wa shule za sekondari na msingi wa Halmashauri ya wilaya ya Uyui mkoani Tabora, wamelalamikia dhuluma na udhalimu unaofanywa na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi.
Wamemtaka Waziri wa wizara hiyo, Dk. Shukuru Kawambwa, kuhakikisha wanalipwa mishahara yao badala ya kuwaacha wakiishi maisha magumu.


Wakizungumza juzi walimu hao walisema baadhi yao hawajalipwa malimbikizo yao kwa zaidi ya miaka kumi.
Mbali na hilo, walisema walimu wapya walioajiriwa mwaka huu, hawajalipwa mishahara kwa sababu hawajaingizwa kwenye mfumo wa malipo.
Pia wamelalamikia kukatwa sh. milioni tano bila ya ridhaa yao kwa ajili shughuli ya mbio za mwenge.
Walisema walimu 144 waliajiriwa na kupangiwa kufundisha kwenye shule za sekondari, ambapo 122 ndio walioripoti na kwamba walioingizwa kwenye mfumo wa malipo ni 29.
“Halmashauri ilitukata sh. 5,000 kila mwalimu,  ambazo ziliandikwa ni mchango wa Tabora na tumefuatilia tokea tulipoanza kukatwa mwaka 2010, lakini kila mwaka tunaambiwa tuandike barua ya madai bila majibu,” alisema mwalimu Sivian.
Alisema baadhi ya walimu walioajiriwa mwaka huu, hawajalipwa kutokana na majina kutoingizwa kwenye mfumo wa malipo na kusababisha kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Alisema walimu wa shule za msingi walioajiriwa walikuwa ni 52 na kwamba, walioingizwa kwenye utaratibu wa malipo ni 29.
Kwa upande wake, mwalimu Julius Jotoma alisema walimu wengi walioajiriwa mwaka huu, hawana fedha kutokana na ukiritimba na uzembe unaofanywa na Wizara ya Elimu, Hazina na TAMISEMI.
Mwalimu Magnalena Kileo, aliilalamikia Wizara ya Elimu kwa kutowalipa kwa wakati fedha za safari wakati wa likizo ya mwezi wa sita na ya mwisho wa mwaka.
Alisema inachukua muda mrefu walimu hawapandishwi madaraja na kwamba wakipandishwa, wizara haifuati maelekezo kutoka Tume ya Utumishi wa Umma.
“Tunaomba serikali itusaidie mlolongo wa kupandishwa madaraja, walimu wamekaa tangu mwaka 2001 mpaka sasa wakati kupanda daraja ni miaka mitatu kazini,” alisema.
Ofisa Elimu wa Halmashauri hiyo, Ester Mwangamila, alisema walimu walikatwa fedha hizo na manispaa kwa ajili ya mbio za Mwenge na kwamba suala hilo linashughulikiwa.
“Tulikubaliana na manispaa kuwa, utakapokuja Mwenge, walimu wachangie  kwa atakayekuwa nacho, baadaye nikasikia wamekatwa walimu wote bila ya ridhaa yao, ila tunalishughulikia, suala hilo, liko kwa Ofisa Utumishi wa Manispaa” alisema.
Kuhusu walimu wapya kutolipwa mishahara yao, tangu waajiriwe, Ester alisema amefuatilia suala hilo mpaka wizarani na kwamba aliambiwa majina yao hayajaingizwa kwenye mfumo wa malipo.
Ester alisema madai ya walimu wa wilaya hiyo ni sh. milioni 19 na yameanza kulipwa na mchakato wa kuhakiki madeni unaendelea kwa walimu wengine.
Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana alisema matatizo ya walimu ni makubwa na hayalingani na matatizo ya watumishi wengine.
Alisema walimu wanaonewa na haiwezekani wakatwe mishahara bila ya ridhaa yao kwa ajili ya Mwenge.
Kinana alisema atazungumza na Waziri wa Elimu, Dk. Shukuru Kawambwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, ili waweze kulipatia ufumbuzi suala hilo.
Alisema serikali imetenga sh. bilioni 60 kwa ajili ya kuwalipa walimu na kwamba kutokana na mlolongo mrefu wa kuhakiki madai ya walimu,watazidi kucheleweshwa na kusababisha madeni kuongezeka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru