Wednesday 28 May 2014

Libya hakukaliki-Membe


NA TUMAINI MSOWOYA, DODOMA
SERIKALI imewashauri Watanzania kusitisha safari zao za kwenda nchini Libya, mpaka hapo watakapotangaziwa vinginevyo, kutokana na kuwepo kwa hali tete ya kiusalama nchini humo.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, alisema hayo bungeni mjini Dodoma jana, alipokuwa akiwasilisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Bernard C. Membe, Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa K'taifa

Membe alisema Watanzania hawapaswi kwenda Libya kwa sasa, kutokana na hali ya kiusalama ya nchi hiyo, ikiwa ni pamoja na kushika kasi kwa mauaji ya raia.
Alisema tangu kuuawa kwa kiongozi wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi,  miaka mitatu iliyopita, pamoja na Balozi wa Marekani nchini Libya,  mauaji ya wenyeji na raia yamekuwa yakiongezeka kutokana na mapigano ya wenyewe kwa wenyewe.
Membe alisema hali ya nchi hiyo imekuwa mbaya zaidi kiasi cha kusababisha waziri mkuu wa nchi hiyo kutekwa nyara na baadaee kuachiliwa na bunge kuvamiwa na kuchomwa moto.
Alisema hali hiyo imezifanya ofisi nyingi za balozi kufungwa kutokana na mauaji hayo na kuifanya Libya isitawalike.
ìTunawashauri Watanzania wasiende Libya kwa sasa kutokana na hali iliyopo mpaka pale serikali itakaposhauri vinginevyo,îalisema Membe.
Kuhusu mgogoro wa Tanzania na Malawi, Membe alisema msimamo wa Tanzania ni kwamba mpaka kati yake na nchi hiyo upo katikati ya Ziwa Nyasa.
Alisema mazungumzo ya usuluhishi wa mgogoro huo yanaendelea na kwamba, serikali inaandaa hoja nzito na zenye ushawishi kuhusu mpaka huo.
Waziri Membe alisema kinachosubiriwa kwa sasa ni kikao, ambacho kitaitishwa na jopo la usuluhishi ili kuendelea na usuluhishi kutokana na mchakato wa uchaguzi na kuundwa kwa serikali mpya ya Malawi.
Kuhusu mapambano dhidi ya ugaidi, Membe aliwataka Watanzania kuendelea kulinda amani na utulivu kwa kutokubali kusuluhisha baadhi ya mambo kwa njia za kigaidi.
Alisema vitendo vya kigaidi vinavyofanywa na kikundi cha Boko Haram nchini Nigeria na Al-shaababu nchini Kenya, havivumiliki na kwamba serikali imeshatuma salamu za pole na utayari wake katika kushirikiana kwenye mapambano dhidi ya ugaidi.
Kuhusu  Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), alisema Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kushiriki kulinda amani, usalama na demokrasia kwenye nchi za kusini mwa afrika, ikiwemo DRC.
Alisema kutokana na msimamo huo, Tanzania imechangia kikosi kimoja cha askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ),  kwenye FBI, iliyoko chini ya kikosi cha Umoja wa Mataifa (UN) cha kulinda amani.
Waziri alisema kikosi hicho kimesaidia kukisambaratisha kikundi cha waasi wa M23, ambao wamekuwa wakivuruga amani kwa muda mrefu Mashariki ya DRC.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru