Sunday 25 May 2014

Ajira mpya laki saba kuzalishwa

NA THEODOS MGOMBA,DODOMA
WIZARA  ya Kazi na Ajira inatarajia kuzalisha ajira 700,000 katika mwaka wa fedha wa 2014/2015.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Waziri Gaudentia Kabaka alipokuwa akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake.

Gaudentia alisema ajira hizo zitatokana na utekelezaji wa miradi ya maendeleo itakayotekelezwa na taasisi za umma, programu ya kukuza ajira kwa vijana na hatua mbalimbali za uwekezaji.

Waziri alisema hadi kufikia Aprili mwaka huu, ajira 630,616 zilizalishwa katika mwaka wa fedha unaoishia mwezi ujao.

Alisema ajira hizo zilizalishwa katika sekta za kilimo (130,974), elimu ajira (36,073), ujenzi na miundombinu ajira (32,132) nishati na madini ajira 453,  afya ajira 11,221, TASAF ajira 8,686 na sekta nyingine serikalini ajira 2,321.

Sekta nyingine ni sekta binafsi ajira 211,970, viwanda vidogo na vya kati (SMEs) ajira 7,192, miradi ya uwekezaji kupitia maeneo huru ya uwekezaji -EPZ ajira 26,381, mawasiliano ajira 13,619 na miradi kupitia Kituo cha Uwekezaji Tanzania  (TIC) ajira 149,594.

Gaudentia alisema wizara kwa kushirikiana na Shirika la Kazi Duniani (ILO) inaendelea na juhudi za kuwajengea vijana uwezo wa kuwawezesha kujiajiri wenyewe katika maeneo yao.

Alisema mafunzo ya ujasiriamali  yametolewa kwa vijana 11,500 kupitia Mradi wa Kazi Nje Nje katika mikoa 17 ya Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Waziri Gaudentia mafunzo hayo yalilenga katika kubadili fikra za vijana  kuwa ajira ni pamoja na kujiajiri, kuwajengea uwezo vijana katika kutambua fursa zilizopo, namna bora ya kuandaa miradi, kutafuta masoko na kutunza hesabu za biashara.

Alisema ili kukuza ajira na kazi za staha nchini, wizara itaratibu uingizaji wa masuala ya ukuzaji ajira katika mipango na programu za maendeleo za kisekta kwa kutoa mafunzo katika mikoa mitatu.

Pia, katika mwaka ujao wa fedha  pamoja na programu hizo,  wizara itafuatilia utekelezaji wa mwongozo wa namna ya kuhuisha ukuzaji ajira nchini.

Alisema wizara itaendelea kufanya utafiti wa hali ya nguvu kazi ambao utatoa picha ya hali ya ajira nchini.

Waziri Gaudentia alisema utafiti huo utatoa taarifa kuhusu ajira katika sekta rasmi na isiyo rasmi, hali ya utumikishwaji wa watoto na idadi ya ajira mpya zilizozalishwa katika kipindi cha mwaka 2006 hadi 2014.

Alisema katika mwaka ujao wa fedha  serikali inatarajia kuzuia watoto 4,000 kuingia kwenye ajira mbaya na kuwaondoa watoto 10,000 wanaotumikishwa kwenye ajira mbaya.

Akichangia hutuba hiyo, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maendeleo ya Jamii, Said Mtanda alisema ni vyema serikali ikakamilisha mchakato wa uanzishwaji wa Mfuko wa Pensheni ya Wazee.

Alisema kuanzishwa kwa mfuko huo kutasaidia wazee waweze kuboreshewa hali zao za kimaisha.

Mtanda alisema kumekuwa na mitazamo mingi tofauti ikiwa ni pamoja na mtazamo kuwa wazee ambao hawakuchangia kuweka akiba katika mfumo rasmi hawawezi kulipwa pensheni.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru