Thursday 8 May 2014

Zitto awalipua wabunge



  • Asema wapo wanaotumiwa na wafanyabiashara
  • Lengo ni kukwamisha kufutwa misamaha ya kodi

Na theodos mgomba, Dodoma
MBUNGE wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema kuna mchezo mchafu unaotaka kufanywa na wafanyabiashara wakubwa kwa kushirikiana na baadhi ya wabunge.

Mchezo mchafu huo unalenga kuhujumu uwasilishaji wa Muswada wa kufuta misamaha ya kodi nchini, ili waendelee kuikwamisha serikali isikusanye mapato yake kikamilifu.
Zitto, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali, alisema kuna kundi la wafanyabiashara wameungana ili kuhakikisha muswada huo unakwama kuwasilishwa bungeni.
Aliyasema hayo alpokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, baada ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, kuwasilisha taarifa yake.
Alisema katika kuhakikisha muswada huo unakwama, baadhi ya wafanyabiashara wamekuwa wakihaha kuwaweka sawa baadhi ya wabunge ili kusaidia harakati hizo.
“Kuna baadhi ya wafanyabiashara wakubwa na wengine wenye kampuni kubwa zikiwemo za kuchimba madini, wanahaha ili kukwamisha muswada huo usije bungeni. Tunaomba tushirikiane kuzima hujumu hizi ambazo zinalenga kukwamisha juhudi za serikali.
“Tunapoteza zaidi ya sh. bilioni 40 katika misamaha ya kodi hivyo, hizi ni fedha ambazo zingeweza kufanya kazi zingine za kijamii.”
Pia, alitumia fursa hiyo kuhimiza matumizi ya mashine za kieletroniki (EFD) kwa wafanyabiashara na kuongeza wigo wa matumizi yake katika malipo mbalimbali ya serikali.
“Kuna umuhimu mkubwa wa kutumika kwa mashine hizi kwa wafanyabiashara, lakini ni vyema serikali pia ikaanza kuzitumia katika manunuzi yake mengine,’’ alisema Zitto.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru