Wednesday 14 May 2014

Mwanza mwenyeji tuzo za mazingira


NA PETER KATULANDA, MWANZA
HALMASHAURI ya Jiji la Mwanza, imepewa heshima ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya Tuzo za Usafi na Mazingira nchini, inayotarajiwa kufanyika Juni 5, mwaka huu.
Maadhimisho hayo huratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, (TAMISEMI), kabla ya kutolewa na Ofisi ya Makamu wa Rais Mazingira.
Wakati Jiji hilo likijiandaa na maadhimisho hayo, Meya wake, Stanslaus Mabula, amemtaka Mbunge wa Nyamagana, Ezekia Wenje, kuacha kuwachochea wafanyabiashara wadogo (Wamachinga) wavunje utaratibu, kanuni na sheria za Mipango Miji.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mwanza, Halfa Hida, alisema juzi kuwa ofisi ya Waziri Mkuu imeisha toa vigezo vya kushindaniwa na Majiji, Manispaa na Halmashauri za wilaya nchini.
Aliwataka Madiwani, Watendaji wa Kata na Mitaa, kuendelea kuweka mazingira katika hali ya usafi ili jiji hilo liibuke tena na tuzo ya ushindi kwa mara ya tisa mfululizo.
“Tutumie sheria ndogo za halmashauri yetu na kuhamasisha wananchi na vikundi vya usafi kuweka mazingira katika hali ya usafi kabla ya wakaguzi kupita kwenye mitaa na kata, kutoa alama,” alisema.
Huku akitamba kunyakua ushindi kwa mara ya tisa, Hida, aliwaagiza maofisa afya kuweka mikakati ya kuendeleza usafi katika jiji hilo, aliloliita ‘Smart City’ ili kuvutia wawekezaji na wageni. 
Alisema wageni kutoka majiji na miji ya nje ya nchi, wanakaribishwa kushiriki katika maadhimisho hayo.
Meya, Mabula, akihutubia Baraza la Madiwani wa jiji hilo, alisema licha ya Wenje kutoshiriki mara kwa mara katika vikao hivyo, amekuwa akiwahamasisha wamachinga na wafanyabiashara wengine kufanya biashara katika maeneo yasiyoruhusiwa, jambo linaloweza kusababisha kupoteza ushindi.
Aliwataka madiwani na wataalamu wa afya waendelee kusimamia mpango kamambe wa Usafi na Mazingira wa jiji hilo.
Mpango huo ulizinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Mhandisi Evarist Ndikilo, ambao hutekelezwa kila mwanzoni mwa wiki ya kwanza ya kila mwezi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru