Thursday 15 May 2014

MoEVT yaingilia kati madai ya walimu


NA WILLIAM SHECHAMBO
WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi (MoEVT), imesema itapambana kuhakikisha inatatua kero za walimu hususan madai yao, kwasababu inaamini ndio ufunguo muhimu wa mafanikio kwenye Mpango wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Imesema kwa kuanzia, inafanyakazi kwa karibu na mashirika ya maendeleo duniani na binafsi yaliyopo nchini, ili kuweza kupata rasilimali zitakazotoa utatuzi kwa kero za muda mrefu zinazo wakabili walimu.
Akizungumza na wafanyakazi wa Wizara yake kwenye mkutano wa 22 wa wafanyakazi jana, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, alisema madeni ya walimu yamepewa kipaumbele kwenye mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN).
Kawambwa, alisema Serikali kupitia wizara yake, imetia saini makubaliano ya kupewa ruzuku ya dola za Marekani milioni 94.8, kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Ushirikiano wa Elimu (GPE), fedha ambazo zitaingia kwenye BRN.
Pia, alisema jumla ya sh. milioni 500 zinatolewa na serikali kila mwaka kwenye halmashauri 40 nchini kwa awamu ya kwanza, ambazo zimedhamiriwa kujenga nyumba za walimu kwenye maeneo ambayo yamekosa kabisa.
Aidha, alisema wizara yake imeonyesha nia ya kuwajali walimu kuhusiana na matokeo ya mitihani ya taifa, kwa kutoa mtihani maalum wa darasa la pili uliozingatia kusoma, kuhesabu na kuandika (KKK).
Alisema lengo ni kutaka kupeleka kizazi cheye uelewa ambacho kitatoa matokeo makubwa ya elimu ya msingi na sekondari katika miaka ya usoni. 
Waziri huyo, aliwaambia wafanyakazi wa MoEVT kuwa lazima wajitahidi kubadilika kwenye utendaji ili kufanikiwa katika  mipango mbalimbali ya kujenga, hususan BRN.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru