Wednesday 14 May 2014

Nyalandu apangua hoja za wabunge


NA THEODOS MGOMBA, DODOMA
WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Lazaro Nyalandu, jana alifanikiwa kupangua hoja moja baada ya nyingine zilizotolewa na wabunge wakati wakichangia hotuba ya Makadirio ya Matumzi ya wizara yake, kwa mwaka wa fedha 2014/2015, huku akisitiza kuwa baadhi ya uamuzi alioutoa kuhusu watendaji wa wizara hiyo utabaki kama ulivyo.


Akijibu hoja hizo, Nyalandu alisema kuna hoja nyingi ambazo zimeelekezwa kwake binafsi na zingine kwa wizara, huku nyingi zikiwa ni za uzushi ambazo zimepikwa na watu wachache wasio na mapenzi mema kwa taifa.
Alisema moja ya hoja hizo ni ya habari kuwa amemfukuza kazi Mkurugenzi wa Idara ya Wanyamapori, Profesa Alexander Songorwa.
Alisema jambo hilo halina ukweli na alichokifanya ni mabadiliko ya kawaida ya vituo vya kazi.
Nyalandu, alisema mabadiliko hayo yamefuata utaratibu na hakuna aliyefukuzwa kazi kama ilivyodaiwa na baadhi ya watu na vyombo vya habari.
“Mheshimiwa Sakaya (Magdalena – CUF), dada yangu umesema kwa emotion… (hisia) lakini ukweli, hakuna mtendaji aliyefukuzwa kazi bali wamehamishwa vituo.
“Profesa Songorwa anakwenda Chuo cha Mweka, ni chuo chenye heshima, mwingine Jafari Kidegesho, anakwenda kwenye Mbuga ya Selous ambako anakwenda kuwa kiongozi namba mbili, hivyo hakuna aliyefukuzwa,’’ alisema.
Awali, akichangia hoja hiyo, Magdalena alisema watendaji hao wamedhalilishwa kwa kufukuzwa kinyume cha utaratibu.
Pia, alimtuhumu Nyalandu kuwa hatua yake hiyo inaweza kuwavunja moyo wana taalamu wengine nchini, ambao wamekuwa wakijitolea kusaidia masuala mbalimbali.
“Waziri amewadhalilisha hawa wanataaluma kwa kuwafukuza kazi bila kufuata utaratibu wa utumishi, nataka kusikia kama yuko tayari kuwaomba radhi na kuwarudisha kwenye nafasi zao za zamani,
Hata hivyo, Nyalandu alisema uamuzi wake kuhusu watendaji hao utabaki kuwa hivyo na hakuna kitakachobadilika.
Kuhusu Operesheni Tokomeza Ujangili, Nyalandu, alisema Rais Jakaya Kikwete alishaunda Tume ya Mahakama ambayo itafuatilia mambo yaliyojitokeza wakati wa utekelezaji wake.
Alisema kwa sasa hana jibu zuri la kutoa bungeni hadi pale Tume hiyo itakapokamilisha kazi yake na kutoa taarifa.
Kwa upande wa suala la kwenda Afrika Kusini, Nyalandu alikiri kwenda baada ya kutumwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda.
Alisema sababu kubwa ya kwenda huko ni ilikuwa kuonana na Bodi ya Hifadhi ya Mbuga ya Afrika, ili kujua utendaji kazi wake na kuona kama Tanzania inaweza kujiunga na Bodi hiyo katika kulinda hifadhi zake.
Alisema pia ilikuwa kwenda kujua jinsi gani bodi hiyo inafanya kazi na kujua mfumo wake katika utekelezaji wa majukumu yao.
“Sasa hao wanaosema kuwa nilienda kuonana na wawindaji si kweli na waongo, wote sehemu yao ya kuishi ni katika ziwa linalowaka kwa kibiriti,’’ alisema.
Alisema ameshaweka mpango wa watendaji wake kwenda nchi mbalimbali ikiwemo Malawi na Ethiopia, kuona jinsi gani Bodi hiyo imeweza kufanikiwa katika kulinda hifadhi.
Kuhusu lango la Gologonja katika mpaka wa hifadhi ya Serengeti na Masai Mara, Nyalandu alisema, haliwezi kufunguliwa licha ya maombi ya nchi zilizo ukanda wa Afrika Mashariki.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru