Wednesday 14 May 2014

Serikali ya Misri yaisaidia Muhimbili


NA KHADIJA MUSSA
MKURUGENZI Mtendaji wa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Dk. Marina Njelekela, ameiomba serikali ya Misri iwasaidie kusomesha wataalamu katika kitengo cha Urolojia.
Alitoa ombi hilo, kutokana na changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa wa Urolojia nchini, hususan katika Hospitali ya Muhimbili, ambapo kwa sasa wapo wataalamu 20 kwa nchi nzima.
Dk. Marina, aliyasema hayo jana wakati wa kupokea msaada wa vifaa tiba kutoka serikali ya Misri, ambavyo vinalenga kuboresha kitengo cha Urolojia.
Alisema vitasaidia kuwezesha huduma kutolewa kwa kiwango kinachokubalika.
Dk. Marina, alisema huduma zinazotolewa katika kitengo hicho ni pamoja na uvimbe wa tezi dume, kuziba kwa njia ya mkojo kutokana na kovu, saratani ya kibofu, saratani ya tezi ya kiume na mawe kwenye figo.
Alisema mara nyingi walikuwa wakipokea wataalamu bingwa kutoka Misri ambao hukaa na wataalamu wa hapa nchini na kuwapa ujuzi katika vitengo mbalimbali kikiwemo cha Urolojia.
Dk. Marina, aliiomba serikali hiyo kuwasomesha wataalamu wa hapa nchini ili kukabiliana na changamoto ya upungufu wa mabingwa wa kitengo hicho.
Akizungumzia kuhusu vifaa walivyopokea, alisema watahakikisha vinafanyiwa matengenezo ya mara kwa mara ili viweze kudumu na pia aliahidi kuvitumia kwa malengo yaliyokusudiwa.
“Vifaa tunavyokabidhiwa leo (jana) vitasaidia wagonjwa hasa wale wanaoandaliwa kwenda kufanyiwa upasuaji, walioko chumba cha upasuaji na wale wanaohitaji uangalizi maalumu baada ya kufanya upasuaji,” alisema.
Kwa upande wake Balozi wa Misri nchini, Hossam Moharam, aliipongeza hospitali hiyo kwa utoaji wa huduma bora na aliahidi kuendeleza ushirikiano.
Serikali ya Misri ilikabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya dola 250,000 (sawa na sh. milioni 400).

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru