Sunday 25 May 2014

Migogoro ya ardhi wakulima, wafugaji yawa moto bungeni

NA ABDALLAH MWERI
SAKATA la kuhusiana na migogoro ya ardhi kati ya wakulima na wafugaji nchini, jana ulizua mjadala mzito bungeni
wakati wabunge wakichangia majadiliano kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi.

Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Titus Kamani, juzi usiku aliwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2014/2015.

Sehemu kubwa ya majadiliano ya wizara hiyo yalihusisha zaidi mapigano makali kati ya wakulima na wafugaji katika
maeneo mbalimbali nchini.

Wabunge hao walisema serikali ina wajibu wa kuchukua hatua haraka kwa lengo la kuepusha mapigano ya wakulima na wafugaji ambayo yamesababisha vifo.

Mbunge Benedict Ole Nangoro (Kiteto-CCM) alisema fedha zilizotengwa ya bajeti iliyotengwa katika wizara hiyo haina mashiko kwa kuwa waziri atashindwa kutekeleza majukumu yake kikamilifu.

Alisema Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi ni nyeti, hivyo ilitakiwa kupewa fedha za kutosha ambazo miongoni mwa kazi zake ni kuhakikisha zinatatua migogoro ya wakulima na wafugaji nchini.

Ole Nangoro alisema mbali na fedha ndogo kutengwa katika wizara hiyo, pia serikali inatakiwa kuunda chombo maalumu ambacho kitakuwa wakala wa kushughulikia matatizo ya wakulima na wafugaji.

“Serikali iunde chombo maalumu au wakala kama TANROADS ambacho kitakuwa na mamlaka ya kushughulikia matatizo yote ya wakulima na wafugaji,” alisema Ole Nangoro.

Naye Mahmoud Jumaa (Kibaha Vijiji-CCM), alisema migogoro ya ardhi itaepukwa endapo serikali itatenga maeneo maalumu kwa ajili ya wafugaji.

Pia, alisema ujenzi wa machinjio ya kisasa akitolea mfano katika jimbo lake la Kibaha Vijijini, utapunguza kwa kiasi kikubwa mapigano ya wakulima na wafugaji.

Alisema serikali inatakiwa kujenga machinjio ya kutosha katika maeneo mbalimbali nchihi hatua ambayo itachochea ufugaji wa kisasa ambapo wafugaji watapata fursa nzuri ya kufunga kitaalamu.

Kwa upande wake, Selemani Nchambi (Kishapu-CCM), alisema ili kuepusha mauaji, serikali ina wajibu wa kujibu kwa kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji kwa lengo la kuepusha mapigano.

“Bajeti ya mifugo ni ndogo ni jukumu la serikali kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji ili kuepusha mapigano dhidi ya wananchi katika maeneo mbalimbali kama Kiteto na Kishapu,” alisema Nchambi.

John Cheyo (Bariadi Magharibi-UDP), alisema serikali imechelewa kuchukua hatua kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji nchini, hivyo ameitaka kuchukua hatua haraka ili kukomesha mauaji.

Alisema wafugaji wamekuwa wakihama kutoka eneo moja hadi jingine kwa kuwa serikali imeshindwa kuwajengea uwezo wa kufuga katika mazingira bora.

Ridhiwani Kikwete (Chalinze-CCM), alisema elimu ya kutosha ndiyo njia pekee inayoweza kunusuru mapigano baina ya jamii hiyo.

Mbunge huyo aliitaka serikali kutenga maeneo tofauti ya wakulima na wafugaji sanjari na kujenga kwa wingi majosho na machinjio.

Muhammad Sanya (Mji Mkongwe -CUF) alisema Tanzania ina hazina kubwa ya mifugo na ikitumika vyema itakuwa na uwezo wa kupata fedha nyingi za kigeni.

Sanya alisema endapo wafugaji wataelimishwa kufuga kisasa, Tanzania itapata fedha kutoka Saudi Arabia, Omani, Comoro na nchi zingine zenye uhitaji mkubwa na nyama.

Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM) alisema Tanzania ina hazina kubwa na mifugo, lakini wafugaji wameshindwa kupata faida kutokana na kazi yao kwa kuwa serikali haijatoa elimu ya kutosha.

Kwa upande wake, Lekule Laizer (Longido CCM), alisema migogoro baina ya jamii hiyo imetokana na serikali kushindwa kuchukua hatua stahiki mapema akitolea mfano wa Hifadhi ya Murtangos iliyoko Kiteto, Manyara.

Ziadi ya watu 10 wameuawa katika mapigano makali kati ya wafugaji kutoka Wilaya ya Kiteto na wakulima wa Kongwa, Dodoma ambao wanagombea eneo lililotengwa kwa ajili ya hifadhi tengufu.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru