Friday 9 May 2014

Mnyukano bungeni

 
TASWIRA ya Bunge jana ilibadilika kwa muda pale baadhi ya wabunge walipochepuka kujadili hoja na kuanza kunyukana kwa kurushiana makombora hadharani.
Mnyukano huo ulikwenda mbali zaidi, baada ya Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye, alipoliomba Bunge kuwa na utaratibu wa kuwapima wabunge akili kabla ya kuingia ndani ya ukumbi huo.
Hali hiyo ilimfanya Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai naye kuvunja ukimya na kueleza kuwa kuna baadhi ya viongozi ni wabaguzi jambo ambalo ni hatari na halikubaliki.
Goodluck Ole Medeye
Alisema suala la mgogoro wa wakulima na wafugaji katika eneo la mpakani mwa wilaya ya Kongwa na Kiteto iliyopo mkoani Manyara, halipo, bali linakuzwa na ubaguzi wa baadhi ya viongozi.
Ndugai, ambaye pia ni mbunge wa Kongwa alisema, kati ya wakazi wa jimbo lake na Kiteto, kumekuwa na ubaguzi ambao umekuwa ukisababisha mauaji ya mara kwa mara.
“Kweli dakika saba ni chache kwangu kuchangia, ningekuwa na muda ningezungumza zaidi kuhusu hili, ukweli ni kwamba, kati ya wakazi wa Kongwa na Kiteto kumekuwa na watu wamekuwa wakipoteza maisha.
“Hata usiku (jana), nimekipigiwa simu kupewa taarifa za watu kupoteza maisha, miongoni mwao ni wakazi wa Kongwa.
“Kila siku ni ubaguzi… ubaguzi tu ambao unasababisha mauaji tu, halafu kiongozi anasimama anatetea, anatetea nini hapa,” alisema Ndugai akionyesha hisia kali ya tatizo hilo.
Kabla ya Ndugai kutoa kauli hiyo, mnyukano huo ulianzia kwa Mbunge wa Arusha Mjini (CHADEMA), Godbless Lema dhidi ya Ole Medeye.
Katika mchango wake, Lema alisema kutokea kwa mauaji katika kijiji cha Kimana eneo la Kiteto na watu wawili kuuawa na maduka mawili kuchomwa moto, chanzo ni mgogoro huo uliopo.
Lema alimtuhumu Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Matha Umbula, kuitisha mkutano kijijini hapo kuwataka wakazi wenyeji kukaa upande mmoja, wengine upande mwingine.

“Mheshimiwa Naibu Spika, jana usiku (juzi) kumetokea mauaji kule katika kijiji cha Kimana, watu wawili wameuawa huku maduka na pikipiki 11 zikichomwa moto.
“Inasikitisha kuona aliyeanzisha mauaji haya ni mkuu wa wilaya kwa kuendekeza ubaguzi kwa kuwataka wakazi wa kijiji hicho ambao ni wenyeji kukaa upande mmoja na wale wageni wakae kwingine, huu ni ubaguzi ndani ya nchi hii.
Lema aliendelea kusema, mkuu huyo wa wilaya hana tofauti na Medeye kwa kuendeleza ubaguzi.
Maneno hayo ya Lema yalimfanya Ole Medeye kusimama na kuomba kutoa taarifa kwa Naibu Spika, ambapo alisema kuna haja ya kuwa na daktari wa masuala ya akili ili kujua nani wenye sifa ya kuwemo ndani ya bunge.

“Mheshimiwa Naibu Spika, hii ni mara ya pili Lema anataja jina langu ndani ya bunge hili, Lema ni mtoto wa getho ambaye alitelekezwa na wazazi ndiyo maana anaropoka,’’ alisema Medeye.
Mbunge huyo alisema, daktari huyo wa akili atakapowabaini wenye matatizo ya akili, wasiruhusiwe kuingia ndani ya bunge.
Medeye alisema, yeye ni mzaliwa wa Arusha na akaweka wazi kwamba, katika uchaguzi mkuu ujao mwakani, atajitosa kuwania jimbo la Lema.
Akitoa utetezi wake kuhusu tuhuma dhidi yake, Matha ambaye pia ni mbunge wa viti maalumu, alikiri kufanya mkutano katika kijiji hicho kinachopakana na wilaya ya Kongwa.
Alisema katika mkutano huo, waliotakiwa kuhudhuria ni wajumbe wa halmashauri ya kijiji hicho tu na si watu wengine, ndiyo maana aliwatoa wasiohusika.

“Mheshimiwa Naibu Spika ni kweli nilifanya mkutano huo, lakini waliotakiwa kuhudhuria ni wajumbe wa halmashauri hiyo tu na si watu wengine ndiyo maana nikawaondoa watu wengine, huo si ubaguzi,’’ alisema Matha.
Upepo wa kutuhumiana haukuishia hapo, uliendelea hata aliposimama mbunge wa jimbo la Bukoba mjini, Balozi Khamis Kagasheki.
Mbunge huyo aliilalamikia serikali kwa kutomchukulia hatua za kisheria Meya wa Manispaa ya Bukoba, Dk. Anatory Aman kutokana na matatizo mbalimbali.
Kaghasheki alisema hivi sasa katika halmamshuri hiyo hakuna kinachoendelea kwa sababu kiutaratibu, Meya alishajiuzuru.
Alisema barua kutoka kwa katibu Tawala wa mkoa huo kwenda TAMISEMI nayo ikihoji uwepo wa Meya huyo aliyestaafu.
Kagasheki, aliendelea kusema hata bajeti ya halmashauri hiyo imechomekwa katika bajeti ya mkoa bila hata baraza la madiwani kukaa.

“Naomba kujua leo hapa kama huyo bado ni meya au la, kwani hivi sasa katika halmashauri hiyo hakuna meya,” alisema Balozi Kagasheki.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru