Friday 9 May 2014

UVCCM: JK usiwabembeleze UKAWA

Na Mwandishi wetu
JUMUIA ya Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) Zanzibar, imemuomba Rais Jakaya Kikwete, kuacha mpango wa kuwabembeleza na kuwaangukia wajumbe wa bunge la katiba wa kundi la Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA) ili warejee bungeni.
Umedai kuwa kundi hilo ni la wakimbizi wa hoja lenye agenda ya siri ya kuliyumbisha Taifa.
Msimamo huo ulitangazwa jana na Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar, Shaka Hamdu Shaka, katika mkutano na waandishi wa habari uliofanyika Ofisi Kuu ya Jumuiya hiyo huko Maisara Suleima mjini Unguja.
Shaka alisema UVCCM inaamini Katiba mpya itapatikana bila ya wajumbe wa UKAWA na ikiwa itakosekana theleuthi mbili ya pande mbili za Muungano, hakutakuwa mkosi wala msiba badala yake Katiba ya mwaka 1977 itaendelea kuliongoza Taifa.
Alisema inasikitisha kuona wabunge hao wakikosa ujasiri wa kujenge hoja na kuwashawishi wabunge wenzao kwa weledi wa kuuza fikra na matakwa yao yakubalike badala yake kuamua kukimbia katika uwanja halali wa kisheria na kikatiba na kuzagaa vichochoroni.

“Nia ya UKAWA ni kuleta vurugu, ghasia na maafa kama yaliyotokea Pemba, watu wapate vilema na kupoteza maisha, mkakati wao umekwama, sasa wanatapatapa, nia yao ni kurejea bungeni ili wapate posho, hawana lolote la maana,” alisema Shaka.
Pia, aliponda masharti matatu yaliyotolewa na Mkurugenzi wa Haki za Binadamu na Mawasiliano ya Umma wa CUF, Salum Bimani, aliyeitaka Serikali ikubali matakwa yao ndipo wabunge wa kundi la ukawa warejee bungeni .
“Ni masharti ya kipuuzi, yaliyokosa vigezo, mizania na ulinganifu wa mambo, hayafai kusikilizwa wala kufanyiwa kazi, huu si wakati tena wa kuwabembeleza wajumbe wa CUF, NCCR-Mageuzi na CHADEMA kurejea bungeni, waachwe watange na njia,” alisisitiza Shaka.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru