Thursday 22 May 2014

Mifugo imepunguzwa Ulanga-Mwanry


SERIKALI imetumia sh. milioni 481.731 katika mchakato wa kupunguza mifugo katika wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali na Mitaa(TAMISEMI), Aggrey Mwanry alisema hayo jana bungeni mjini hapa alipokuwa akijibu swali la  Hadji Mponda (Ulanga-CCM).
Mponda alitaka kujua mchakato wa kuhamisha mifugo katika Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga kwa msimu wa kiangazi wa mwaka 2012 na gharama zilizotumika katika mpango huo.
Mwanry alisema kiasi kilichopangwa katika utekelezaji wa mpango huo kilikuwa sh. 85,000,000, ambapo Wizara ya Maliasili na Utalii ilitoa sh. 75,000,000 na Halmashauri ya Wilaya ya Ulanga ilitoa sh. 10,000,000.
Alisema jumla ya sh. 396,731,510 ziliongezeka kwa kuwa muda wa siku nne uliopangwa kwa ajili ya operesheni hiyo haukutosha, badala yake ilitumika miezi mitatu.
Naibu Waziri alisema katika kipindi hicho, ng’ombe waliokuwepo walikuwa 350,000, ambapo kati yao, ng’ombe 285,000 walipunguzwa na kubaki 65,700.
Akijibu swali la Lekule Laizer (Longido-CCM) kuhusu migogoro ya wakulima na wafugaji, Mwanry alisema serikali inafuatilia kwa makini kuhakikisha kila upande unapata haki stahiki kulingana na eneo husika.
Alisema migogoro ya wakulima na wafugaji imekuwa tatizo kubwa, hivyo wizara yake inaendelea na mpango mkakati wa kuhakikisha kila upande unamiliki ardhi yake kwa uhalali.
Naibu Waziri alisema miongoni mwa mikakati ya serikali ni kutoa elimu kwa wakulima na wafugaji ili kuleta amani na utulivu miongoni mwao.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru