Thursday 15 May 2014

Uvujaji nyaraka za serikali ni ujambazi


Na Mwandishi Wetu
UVUJAJI wa taarifa na nyaraka za serikali ni zaidi ya ujambazi, kwa kuwa vitu hivyo vinashirikisha uhalifu wa kimataifa na wa silaha, imeelezwa.


Kauli hiyo ilitolewa hivi karibuni na Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, Cassian Chibogoyo alipotoa taarifa yake kwa vyombo vya habari kuhusu kuibuka watu wanaovamia nyaraka hizo na kuzichapa bila idhini ya serikali.
Chibogoyo aliwahadharisha watu hao akiwataka kuacha tabia hiyo vinginevyo watakabiliwa na mkono wa sheria, ambapo pia aliwataka wachapishaji halali nchini kuzingatia maadili ya taaluma yao.
“Takwimu za dunia hivi sasa zinaonesha kuwa uvamizi wa nyaraka na taarifa za serikali katika mataifa mbalimbali ni chanzo cha kuondoa amani na utulivu katika nchi husika,” alisema Mpiga Chapa huyo mkuu wa serikali.
Alitolea mfano wa udhibiti wa fomu namba TSM9, ambayo hutumiwa na wanafunzi wa shule za msingi kuonyesha uwezo wao na kuweka rekodi ya kuwawezesha kujiunga na elimu ya sekondari.
Alisema fomu hiyo ni muhimu na inahitaji hifadhi ya hali ya juu ili kuchelea kutumiwa vibaya na watu wasio waaminifu.
“Matumizi potofu ya fomu hiyo yanaweza kusababisha kuwapo kundi la wanaojiunga na elimu ya sekondari wakiwa hawana sifa stahiki,” alisisitiza.
Aliongeza kuwa awali fomu hizo zilikuwa zikichapwa holela na wachapishaji mbalimbali katika wilaya na mikoa na kuisababishia serikali matatizo makubwa ya ongezeko la wanafunzi mbumbumbu sekondari, lakini pia kulipia gharama kubwa za uchapaji na kusababisha hasara.
Kutokana na hali hiyo, alisema serikali imerudisha kazi hiyo kwa Mpiga Chapa Mkuu ambaye anasimamia utendaji wote.
“Udhibiti huo wa serikali ndio unaowafanya wachapishaji hao haramu kufikiria kuwa wameporwa maslahi yao na sasa kuanza kutumia baadhi ya vyombo vya habari nchini, kupenyeza nyaraka za serikali na kuvunja sheria na maadili ya kazi yao,” alisema.
Chibogoyo alivitaka vyombo vya habari kuacha kushirikiana na wachapishaji hao haramu, badala yake vijikite katika kutoa elimu ya athari ya kutumia kinyume nyaraka za serikali.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru