Sunday 25 May 2014

Nyambacha: Tunatoa elimu kwa ngazi zote

NA EVA-SWEET MUSIBA
JESHI la Zimamoto na Uokoaji limesema litatoa elimu kwa makatibu wakuu na viongozi wakiwemo wengine wakiwemo wabunge, vyama vya siasa katika ngazi zote ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga ikiwemo moto.
Akizungumza katika kikao cha makamanda wa mikoa kote nchini, kilichofanyika katika Hoteli ya Lamada, Ilala, Dar es Salaam,  Kamishina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Pius Nyambacha, alisema ni muhimu elimu itolewe kwa viongozi hao  ili kuwajengea uwezo wa kukabiliana na majanga na wafahamu majukumu ya Jeshi la Zimamoto na Uokoaji.

Pia , amewakumbusha makamanda hao kujilinda kunapotokea majanga ya moto wawapo kazini.

Alisema jeshi hilo limeanza utaratibu wa kutoa elimu kwa viongozi wake na  viongozi wa kisiasa kote nchini ili kuwahamasisha wananchi wao kujilinda na kujikinga na majanga ya moto yanapotokea.

Tumekuwa tukitoa elimu kupitia vyombo vya habari, lakini sasa tumepanua wigo mpaka kwa viongozi wa ngazi mbalimbali ili kuzuia majanga yasitokee na kuwamahasisha wananchi kutii sheria husika, alisema Nyambacha.

Kuhusu changamoto zinazolikabili jeshi hilo, Nyambacha alisema ni pamoja na uhaba wa vifaa vya kazi kama magari, upungufu wa vifaa vya kuzimia moto, ubovu wa barabara kwa baadhi ya mikoa na msongamano wa magari katika majiji hasa Dar es Salaam na Arusha ambao unachangia kuchelewa kufika eneo la tukio.

Alisema kuwa kanuni ya ukaguzi na vyeti imefanyiwa marekebisho, hivyo  tozo zimepungua kulinganisha na hapo awali na kuna ambazo zimepanda kutoka na ukubwa kwa eneo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru