Tuesday 20 May 2014

Barabara ya Kidatu-Ifakara kuwekwa lami


SERIKALI imeanza  kutekeleza kwa awamu mradi wa ujenzi wa kilometa 178 za barabara ya Kidatu-Ifakara na Ifakara-Mahenge kwa kiwango cha lami.
Naibu Waziri wa Ujenzi, Grayson Lwenge alisema bungeni jana kuwa tayari barabara hiyo imeanza kujengwa kwa awamu katika kiwango cha lami.
Alikuwa akijibu swali la mbunge wa Kilombero (CCM), Abdul Mteketa aliyetaka kujua ni lini barabara hiyo itajengwa kwa kiwango cha lami,
Lwenge alisema kwa kuwa serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo kuwa ni uti wa mgongo wa jimbo la Kilombero, ujenzi wa barabara ya Kidatu-Ifakara umekuwa ukitekelezwa kwa awamu, ambapo awamu ya kwanza zilijengwa kilometa 10 kutoka kijiji cha Kiberege hadi kijiji cha Ziginali, ambapo kazi hiyo ilikamilika mwaka 2006.
Alisema katika awamu ya pili, serikali ilijenga kilometa 6.17 kutoka eneo la Kibaoni hadi Ifakara Mjini, ambapo ujenzi huo ulikamilika mwaka 2008.
Aliongeza kuwa katika awamu ya tatu, serikali imeshaanza kutekeleza mpango wa ujenzi wa kiwango cha lami kuanzia eneo la kutoka Kibaoni hadi Zinigali kwa kilometa 16.8.
Alisema katika mwaka wa fedha 2012/2013, serikali ilipata fedha za msaada kutoka serikali ya Marekani kupitia Shirika lake la Misaada la USAID kwa ajili ya kugharamia kazi ya upembuzi na usanifu wa kina wa barabara ya Mikumi-Kidatu-Ifakara yenye urefu wa kilometa 103.3 ili barabara hiyo ijengwe kwa kiwango cha lami.
Kuhusu utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya Ifakara-Taweta-Madeke kupitia Mlimba kwa kiwango cha lami, alisema serikali imepanga kutekeleza kwa awamu.
Alisema awamu ya kwanza itahusisha upembuzi yakinifu na usanifu wa kina ili kuunganisha sehemu ya barabara iliyojengwa awali kati ya Kihansi na Mlimba.
Alisema taratibu za kumpata mhandisi mshauri wa kufanya kazi hiyo zinaendelea na kwamba kwa sasa serikali itaendelea kuimarisha maeneo korofi ili iweze kupitika kwa urahisi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru