Wednesday 14 May 2014

Kikosi maalumu kudhibiti ujangili


NA CHARLES MGANGA, DODOMA
KATIKA kukabiliana na matukio ya ujangili wa wanyamapori, serikali katika mwaka wa fedha 2014/2015, imeanzisha kikosi maalumu cha dharura (Rapid Response Team) kwa ajili ya kupambana na janga hilo.
Kikosi hicho chenye askari 40, kitakuwa chini ya Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA).
Askari hao wamepewa mafunzo maalumu ya ujasiri na ukakamavu wa kukabiliana na vitendo vya ujangili na uokoaji.
Akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Maliasili na Utalii juzi, Waziri wa wizara hiyo, Lazaro Nyalandu alisema, askari hao wana uwezo wa kushuka kwenye helikopta katikati ya msitu kuwakabili majangili.
Aidha, Nyalandu alisema juhudi za kudhibiti ujangili wa tembo, zimeonyesha hali ya kuridhisha ndani ya hifadhi mbalimbali nchini.
“Mfano, hifadhi za taifa za Tarangile na Ziwa Manyara, hakukuwa na tembo waliouawa katika kipindi cha Februari hadi Novemba 2013,”alisema.
Waziri alisema, katika kipindi kama hicho mwaka 2012, hifadhi hizo zilipoteza jumla ya tembo sita.
Alisema Hifadhi ya Ruaha waliuawa tembo saba kati ya Oktoba hadi Desemba, mwaka jana ikilinganishwa na tembo 57 kipindi kama hicho mwaka juzi.
Nyalandu alisema kwa kushirikiana na wadau, serikali imeandaa mkakati wa kitaifa wa kukabiliana na ujangili na biashara haramu ya nyara.
Alisema mkakati huo umejikita katika kuimarisha intelijensia, kuongeza idadi ya watumishi na matumizi ya teknolojia za kisasa katika kubaini majangili ndani ya hifadhi za taifa.
Hata hivyo, alisema juhudi za kuimarisha ulinzi wa rasilimali za wanyamapori, zimeendelea ambapo siku za doria 54, 574 zimefanywa ndani na nje ya ya mapori ya akiba.
“Tayari jumla ya watuhumiwa 391 wamekamatwa kwa kuhusishwa na makosa mbalimbali ya ukiukwaji wa sheria ya wanyamapori namba 5 ya mwaka 2009,”alisema.
Nyalandu alisema, kutokana na makosa hayo, kesi 277 zimefunguliwa kwenye mahakama mbalimbali, kati ya hizo 123 zenye washitakiwa 164 zimeisha kwa watuhumiwa kulipa faini ya jumla ya sh. 75,686,000.
Alisema kesi zingine 154 zenye watuhumiwa 227, bado zinaendelea katika mahakama tofauti nchini.
Mbali na watuhumiwa kukamatwa, nyara za serikali zilikamatwa ambazo ni meno ya tembo mazima 866 na vipande 1,152, meno ya kiboko 20 na kilo 9, 458 za nyamapori.
Nyara zingine ni ndege hai 15, ngozi 165 za wanyama wa aina tofauti, bidhaa 334 zilizotengenezwa kwa singa na meno ya tembo.
Vifaa na mali zilizokamatwa ni bunduki 1,718, risasi 5,033 za aina tofauti, magari 13, baiskeli 66, pikipiki 11, misumeno 125, mitego ya waya 108, ng’ombe 11, 585, mkaa mifuko 1,530, magogo 857 na mbao 35,144.
Nyalandu alisisitiza kuendelea na utaratibu wa kufanya doria ya pamoja ili kuzuia, kudhibiti na kukabiliana na wimbi la ujangili nchini.
Kuhusu ulinzi dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu, alisema wizara kwa kushirkiana na halmashauri za wilaya, iliendesha siku za doria 696 katika wilaya 19 zilizoathirika kutokana na wanyamapori wakali na waharibifu.
Alisema lengo la doria hizo ni kulinda watu na mali zao dhidi ya wanyamapori wakali na waharibifu.
Ilielezwa watu 11 walipoteza maisha huku ekari 4, 345.82 za mazao zikiharibiwa na wanyamapori hao katika wilaya za Busega, Babati, Monduli, Iringa Vijijini, Tabora, Ilemela na Tunduru.
Kufuatia vifo hivyo, serikali imetoa kifuta machozi cha jumla ya sh. milioni 9.2 kwa familia za waliopoteza maisha na sh. 98, 412, 750 kwa walioharibiwa mazao yao na wanyamapori wakali.
Akizungumzia suala la uanzishwaji wa Mamlaka ya Wanyamapori nchini, alisema wizara inakamilisha taratibu, rasimu ya muundo wa usimamizi na majukumu ya mamlaka, ambayo imetayarishwa kabla ya kuanza rasmi mwaka wa fedha 2014/2015.
Kwa mujibu wa taarifa ya kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii, inayoongozwa na James Lembeli (Kahama- CCM), imebaini kuwepo changamoto mbalimbali kwenye sekta ya utalii nchini.
Moja kati ya changamoto hizo ni baadhi ya hifadhi za taifa kutojulikana hivyo kukosa watalii wa kutosha.
Alisema Hifadhi ya Ngorongoro imenufaika na kujitangaza kwa ushirikiano wa Idara ya Utalii, Bodi ya Utalii (TTB) na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA).
Dk. Hadji Mponda (Ulanga–CCM), alisema pamoja na changamoto kadhaa, ameishauri wizara hiyo kudhibiti mianya ya watu wanaovuna misitu kinyume cha sheria.
“Mianya bado ipo, ikiendelea kudhibitiwa, tutaweza kulinda misitu yetu na kudhibiti uvunaji holela,” alisema.
Rosemary Kirigini (Viti Maalumu CCM), mbali ya kuipongeza wizara kwa mafanikio kadhaa katika baadhi ya maeneo, aliikumbusha kuwepo kwa malimbikizo ya fedha yanayoihusu Hifadhi ya Maswa.
James Mbatia (Kuteuliwa NCCR-MAGEUZI) alishauri sekta ya utalii kupewa kipaumbele kwa lengo la kuongeza watalii watakaoiingizia nchi mapato makubwa.
Zakhia Meghji (Kuteuliwa CCM), alizungumzia lango la Gologonja kuhusu kuendelea kwa mazungumzo kati ya wizara ya Maliasili na Utalii na nchi jirani ya Kenya.
Zakhia, ambaye aliwahi kuongoza wizara hiyo kwa miaka tisa, alisema haoni sababu ya kufunguliwa kwa lango hilo ambalo limefungwa kwa miaka 40 iliyopita.
Alisema kitendo cha kufungua lango hilo, kitapunguza idadi ya watalii wanaoingia nchini kwani lango hilo linaunganisha hifadhi ya Serengeti na Masai Mara.
Alisema, kuendelea kufungwa kwa lango hilo, kunawafanya watalii wanaokwenda kwenye hifadhi ya Serengeti walazimike kuingia nchini kabla ya kwenda Kenya.
Peter Msigwa (Iringa Mjini- CHADEMA), alikumbusha kuundwa kwa bodi katika hifadhi za Ngorongoro na TANAPA kwani kutokuwepo kwake  ni kuruhusu mianya ya upotevu wa mapato.
“Tunaomba michango tunayoitoa serikalini muifanyie kazi kwa sababu tunapata taarifa katika mazingira magumu,” alisema Msigwa.
Aliendelea kushauri hifadhi ya Ruaha kutangazwa kwani watalii hushindwa kufika Iringa kwa kutoifahamu ipasavyo kama zilivyo zingine.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru