Tuesday 20 May 2014

Wabunge wataka tume kuporomoka kwa elimu


NA ABDALLAH MWERI, dodoma
SERIKALI imetakiwa kuunda tume maalumu ya wataalamu waliobobea katika masuala ya elimu ambayo itachunguza kwa kina kuporomoka kwa taaluma hiyo nchini.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na wabunge wakati wakichangia mapitio ya utekelezaji wa bajeti ya makadirio ya mapato na matumizi katika Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi katika mwaka wa fedha 2014-2015.
Akichangia makadirio ya mapato na matumizi katika wizara hiyo, Peter Serukamba (Kigoma Mjini-CCM), alisema mfumo wa elimu nchini uko ‘ICU’, hivyo ameitaka serikali kuunda tume maalumu ya kutafuta majibu ya tatizo hilo.
Alisema hatua ya serikali kuunda tume si jambo jipya kwa kuwa baadhi ya mataifa makubwa duniani yaliwahi kuunda tume zao kwa ajili ya kutatua tatizo la elimu lililokuwa likizikabili nchi zao.
“Elimu yetu iko katika hali mbaya. Ni vyema tukaacha siasa na kujikita katika kutafuta ufumbuzi wa tatizo kwa kuwa kwa miaka mingi limeshindwa kupatiwa majibu,” alisema Serukamba.
Naye James Mbatia (mbunge wa kuteuliwa) alisema Rais Jakaya Kikwete, aunde tume ya kudumu ya wataalamu waliobobea katika sekta ya elimu nchini, ambayo itafanya utafiti wa kina kubaini sababu ya kuporomoka kwa elimu nchini.
Mbatia alisema tume hiyo inatakiwa kujikita katika kusimamia ubora wa elimu, kuhariri vitabu, kuboresha mitaala na kufanya uamuzi kuhusu sekta ya elimu.
Jason Rweikiza (Bukoba Vijijini-CCM), aliitaka serikali kujenga mfumo imara wa ukaguzi wa shule ambao utakuwa na tija katika kutoa elimu bora.
Alisema suala la ukaguzi limekuwa na changamoto kubwa na limechangia kudumaza kiwango cha elimu nchini kwa kuwa shule nyingi hazina ubora stahiki.
Rweikiza alisema ukaguzi wa mara kwa mara utaleta tija kwa wanafunzi kupata elimu bora kulinganisha na sasa ambapo, mfumo huo umeshindwa kutekelezwa muda mrefu.
Mbunge huyo, ambaye ni mmiliki wa shule nane nchini, alitolea mfano wa shule zake kwamba mara ya mwisho zilifanyiwa ukaguzi mwaka 2005.
Deo Ntakumazina (Ngara-CCM), aliitaka wizara kufanya utafiti kuhusu mfumo wa elimu na ikiwezekana kuongeza idadi ya masomo ili kupata wanafunzi wenye upeo wa kutosha.
Ntukamazina alisema hakuna mgawanyo sawa wa walimu kwa kuwa ziko baadhi ya shule zina idadi kubwa ya walimu katika masomo ya sayansi kulinganisha na zingine na alitolea mfano shule za kata.
Betty Machangu (Viti Maalumu-CCM) alisema wizara hiyo imeshindwa kutekeleza ahadi zake kwa sababu bajeti yake imekuwa ikipungua mwaka hadi mwaka.
“Hatuwezi kuwa na elimu bora wakati kila mwaka bajeti ya wizara hii imekuwa finyu. Mwaka 2008 ilipunguzwa kwa asilimia 20 na mwaka 2011-2013 imeshuka hadi asilimia 17,” alisema Machangu.
Peter Msolla (Kilolo-CCM) alidokeza kuwa, walimu wa sayansi ni tatizo kubwa na limechangia kiwango cha elimu kusuasua.
Pia, alisema wizara hiyo imeshindwa kufanya kazi zake kwa ufanisi kwa kuwa inabeba mzigo mkubwa wa wanafunzi wa shule za msingi hadi vyuo vikuu.
Msolla aliitaka wizara hiyo kutenganishwa kati ya Elimu ya Juu na shule za msingi na sekondari ili kutoa fursa kwa watendaji kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
Alisema mwaka 2013, walimu 29,000 walipendekezwa, wa sayansi walikuwa 2,000 na mwaka huu 36,000, kati yao chini ya 2,000 ni wa sayansi.
Kwa upande wake, Margereth Mkanga (Viti Maalumu-CCM) ameitaka serikali kuwasomesha bure wanafunzi wenye tatizo la ulemavu ili kuleta uwiano sawa.
“Kwa kweli naumia sana, watoto wenye ulemavu wanapata shida sana. Kwanini serikali isichukue jukumu la kuwasomesha bure. Katika hotuba ya wizara, hakuna sehemu inayoonyesha watu wenye ulemavu wamepewa nafasi,” alisema Margareth.
Chacha Nyambari Nyangwine (Tarime-CCM) aliitaka serikali kuvipeleka vyuo vya VETA katika wizara ya Elimu, Teknolojia na Mawasiliano kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kuleta ufanisi.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru