Wednesday 28 May 2014

Saba mbaroni kwa mauaji ya askari


Na Moses Mabula, Tabora
POLISI mkoani Tabora, imewatia mbaroni watu saba wanaotuhumiwa kuhusika katika mauaji ya askari polisi wawili kwa kuwapiga risasi.
Tukio hilo la uhalifu, lilitokea hivi karibuni katika kijiji cha Usoke wilayani Urambo mkoani Tabora.
Watuhumiwa hao walikiri kuhusika na mauaji hayo, pamoja na matukio mengine ya uhalifu na unyang`anyi wa kutumia silaha, likiwemo tukio la Aprili 28, mwaka huu, ambapo askari hao walipoteza maisha.
Kamanda wa Polisi mkoani Tabora, Suzan Kaganda, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Silvester Mussa, maarufu kwa jina la Kindwendu(31), mkazi wa Mkuyuni Tambukareli, Mwanza, Sadiki Hamisi, maarufu kwa jina la White, mkazi wa mtaa wa Mihogoni mjini Tabora na Abeli Benedict, mkazi wa Muungano, Urambo.
Wengine ni Fransic  Masanja (38), mkazi wa Nansio, Ukerewe mkoani Mwanza, Haji Athumani (50), mkazi wa Usoke, Urambo, Mussa Khatibu (49) na Ramadhani Kassimu  maarufu kwa jina la Rama Manywele, wakazi wa Tabora.
Susan alisema watuhumiwa hao walikamatwa wakiwa na bastola na risasi tano. Alisema walipohojiwa, walikiri kuitumia bastola hiyo katika matukio ya uhalifu.
Kamanda huyo alisema baada ya kuwahoji, watuhumiwa hao walikiri kuhusika na  matukio ya uhalifu wa kutumia silaha, likiwemo tukio hilo la kuuawa kwa askari namba  F.5179 PC, Jumanne na namba G. 3388, PC Shabani.
Askari hao wa kituo cha polisi cha Usoke, waliuawa katika majibizino ya risasi katika tukio la uporaji  katika nyumba ya mmoja wa wafanyabiashara wa kijiji hicho mwishoni mwa mwezi uliopita.
Mbali na watuhumiwa hao , alisema wamemtia nguvuni mtuhumiwa mmoja, akimiliki silaha kinyume cha sheria na kuitumia katika vitendo mbalimbali vya uhalifu.
Wakati huo huo, watu 17 wamekamatwa na polisi katika wilaya za Kaliua, Igunga, Nzega na Manispaa ya Tabora kwa tuhuma za kupatikana na gunia sita na kete 402 za bhangi na lita 110 za pombe haramu aina ya Gongo.
Kamanda Suzan alisema watuhumiwa hao wanatarajiwa kufikishwa mahakamani wakati wowote baada ya upelelezi wa polisi kukamilika.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru