Thursday, 22 May 2014

Mbowe, Slaa wapewa siku 14 kujitoa UKAWA

Na Hamis Shimye
WANACHAMA wa CHADEMA wameupa siku 14 uongozi wao wa juu kujitoa katika muungano wa Umoja wa Kutetea Katiba ya Wananchi (UKAWA).


Pia wametaka Baraza Kuu la Uongozi la chama hicho, liitishwe na lisimamiwe na baraza la wazee na si uongozi uliopo kwa kuwa umeonyesha ni watu wenye uchu wa madaraka.
Tamko hilo lilitolewa jana mjini Geita na Katibu wa BAVICHA mkoani Geita, Fikiri Migiyo, ambaye pia ni Mjumbe wa Baraza Kuu na Mkutano Mkuu wa chama hicho.
Migiyo alitoa tamko hilo, kwa niaba ya wajumbe wenzake wa baraza kuu na mkutano mkuu katika mikoa ya Geita, Mwanza, Simiyu na Kagera.
Alisema wanaungana na kuwapongeza wajumbe wenzao wa mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Tanga kuukemea upuuzi huu wa UKAWA.
“Suala hili halipaswi kuvumiliwa na ninawaomba wanachama wenzangu katika mikoa mingine, wasimame na wakemee kwa pamoja kuondoa upuuzi huu,’’ alisema.
Migiyo alisema CHADEMA ni chama makini kinachoamini katika nguvu ya umma na sio nguvu ya viongozi, ambao wameendelea kuwaburuza  wanachama.
Alisema viongozi wa ngazi za chini ndani ya CHADEMA wanaburuzwa bila kushirikishwa katika maamuzi ya chama.
“Tunalaani kwa nguvu zote kitendo cha viongozi wetu wa juu kufanya maamuzi ya kihuni na ya kifedhuli kususia Bunge Maalumu la Katiba na kujiunga katika umoja wao,’’ alisema.
Kiongozi huyo alisema kuanza kutoa masharti ni mambo ya kitoto na wanapaswa kurudi bungeni ili kuendelea na mchakato huo.
“Tunasikitishwa na unafiki huu uliopitiliza, viongozi wetu wamekubali kuwa sehemu ya matapeli wa kisiasa, wamekwenda kwenye Bunge la Katiba kula posho zinazotokana na kodi zetu walala hoi, halafu wameacha kufanya walichotumwa,’’ alisema.
Alisema kuanzishwa kwa UKAWA na kususia Bunge la Katiba ni muendelezo wa siasa za kinafiki kwa kuwa huu ni muendelezo wa mipango ya kuwahadaa watanzania kupitia misimamo yao.
Hivyo alisema wanautaka uongozi chini ya Mwenyekiti, Freeman Mbowe na Katibu Mkuu, Dk. Wilbroad Slaa kuitisha kikao cha baraza kuu ndani ya siku 14 kuanzia sasa.
Tamko la wajumbe hao, kupinga chama chao kujiunga na UKAWA, limekuja muda mfupi baada ya wajumbe wenzao kutoka mikoa ya Pwani, Dar es Salaam na Tanga kupinga uamuzi huo.

4 comments:

 1. NIVEMA CHADEMA WENYEWE WAMEELEWA NA KUKIRI UPUUZI WA UKAWA

  ReplyDelete
 2. Uhuru -sisiem hatudanganyiki ng'o!!

  ReplyDelete
 3. Hahaha hao vijana wa Masaburi tumewasoma mapema hao ni sisiem ha hili ni gazeti chini ya utawala walo, walilipwa fedha,, kwa bahati mbaya hamko kibiashara msingenunulika kisrahisi but kuna ruzuku

  ReplyDelete
 4. Gazeti la UHURUU is equal to Sisiem

  ReplyDelete