Wednesday 28 May 2014

Wabunge nusura wazichape kavukavu



  •  Ni Keissy wa CCM na Sanya wa CUF
  •  Hoja walizozitoa bungeni zazusha balaa

NA ABDALLAH MWERI, DODOMA
MBUNGE wa Nkasi (CCM), Ally Keissy na mbunge wa Mji Mkongwe (CUF), Mohammed  Sanya, jana  nusura wazichape kavukavu katika viwanja vya Bunge mjini hapa.
Ally Keissy (MB), Nkasi

Chanzo cha wabunge hao kutaka kuzitwanga ni mzozo ulitokea baada ya Keisy  kuwashukia wabunge wa CUF, akidai kwamba wamekuwa wakitoa malalamiko ya kuonewa bila sababu za msingi.
Keissy alisema hayo wakati akichangia hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, ambapo alisema wamekuwa wakilalamika kwamba wanaonewa huku wakiendelea kunufaika na huduma za maji na umeme bila kuchangia chochote kwenye Muungano.
Kauli yake hiyo ilisababisha kuzuka kwa mzozo mkali nje ya ukumbi wa bunge, ambapo Keissy  aliendelea kurushiana maneno makali na Sanya, ambaye alikuwa akijibizana naye kwa hasira kiasi cha kutaka kupigana.
Mzozo huo ulivuta idadi kubwa ya wabunge kutoka vyama mbalimbali, wakiwemo wa CCM, ambao waliingilia kati na kuokoa jahazi kwa kuwatenganisha wabunge hao. Keissy aliondoka katika eneo hilo huku akirusha makombora kwa kambi ya upinzani.
Licha ya kuondolewa katika eneo la tukio, Keissy aliendelea kupiga vijembe akidai kila kukicha wabunge wa upinzani wamekuwa wakilalamika suala la kuonewa bungeni.
“Mmezidi bwana, kuchangia hamchangii, kazi yenu kulalamika tu,” alisema Keissy huku akiondoka katika eneo hilo kwa hasira baada ya kuamuliwa na baadhi ya wabunge.
Akijibu makombora ya mpinzani wake, Sanya, alimtaka Keissy kufunga mdomo, akidai siku zote amekuwa mpinzani katika ustawi wa maendeleo ya Zanzibar.
“Kwenda zako, huna maana wewe, kila siku umekuwa mpinzani wa Zanzibar, tutaonana jioni (ndani bunge),” alisema Sanya na kuungwa mkono na wabunge wenzake wa CUF.
Tukio hilo lilitokea saa 7:03 mchana, nje ya ukumbi wa bunge, mbele ya idadi kubwa ya wabunge, baada ya Naibu Spika, Job Ndugai, kuahirisha shughuli za bunge hadi saa 10: 00 jioni. Tafrani hiyo ilidumu kwa takribani dakika 10.
Kituko hicho kilikuwa kama filamu kwa kuwa kilivuta idadi kubwa ya waandishi wa habari na wafanyakazi wa bunge, ambao walikuwa wamepigwa na butwaa kuhusu tukio hilo.
Tukio hilo liliwagawa wabunge waliolishuhudia kwa kuwa baadhi walisema Keissy alikuwa na hoja ya msingi kwa madai kuwa  wapinzani, hususani wabunge wa CUF, wamekuwa wakipinga Muungano na wengine walimtetea Sanya.
Awali, Kombo Khamisi Kombo (Mgogoni-CUF),  alisema Zanzibar imekuwa ikibaguliwa katika suala la balozi na wafanyakazi katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.
Kombo alidai kati ya mabalozi 35 wa Tanzania, Zanzibar imetoa mabalozi wanne, hatua aliyodai ni upendeleo. Pia alisema wafanyakazi wengi wanaofanya kazi katika balozi za nje ya nchi, wanatoka Tanzania Bara.
Kwa upande wake, Keissy baada ya kupata fursa ya kuchangia, alisema Zanzibar ina wananchi wachache, ikilinganishwa na Tanzania Bara na kwamba imekuwa haichangii katika wizara hiyo kwa zaidi ya miaka 20.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru