Thursday 22 May 2014

Wabunge waitaka serikali ipunguze msongamano Dar



  •  Washauri kuwepo na tozo ya barabara kwa wanaokwenda mjini
  •  Filikunjombe amfagilia Magufuli, asema ni mtendaji kazi makini

NA THEODOS MGOMBA,DODOMA
SERIKALI imeshauriwa kuweka mkakati wa kitaifa kwa kukopa fedha kutoka vyombo vya fedha vya ndani na nje  kwa ajili ya kutatua tatizo la msongamano katika Jiji la Dar es Salaam.
Pia imeshauriwa kuweka tozo ya barabara ili kupunguza watu wanaokwenda mjini bila kuwa na kazi maalumu na badala yake kwenda kupiga mizinga.
Kauli hiyo ilitolewa jana na mbunge wa Ilala (CCM), Mussa Azzan Zungu alipokuwa akichangia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ujenzi.
Zungu alisema ni vyema serikali ikakopa kutoka vyombo vya fedha vya ndani au nje ili kuboresha miundombinu, hususani barabara ili kupunguza msongamano uliopo hivi sasa.
Alisema serikali haina haja ya kuogopa kukopa kwani mara baada ya miundombinu kukamilika, mkopo huo unaweza kujilipa kutokana na kodi mbalimbali, ikiwemo ya barabara na majengo.
“Kama ilivyofanya kwa mji wa Dodoma, serikali ikope hata sh. bilioni 400 tu kwa ajili ya kazi hiyo na mkopo utajirejesha wenyewe kwani kama mtu akiona maboresho yamefanyika, hawezi kukataa kulipa,” alisema.
Zungu alisema pia kuwa ni vyema kukawa na utaratibu wa kulipia gharama za barabara ili kupunguza idadi ya watu wanaokwenda katikati ya mji bila ya kuwa na sababu.
ìEndapo kutakuwa na kodi, kila anayetaka kuingia mjini ni lazima alipe, basi wale ambao hawana kazi mjini hawawezi kwenda na hivyo kupunguza msongamano,”alisema.
ìWapo wengine wanakwenda mjini hawana cha kufanya, wanakwenda kupiga mizinga tu, sasa watu kama hawa hawataweza kwenda kwani hawatakuwa na fedha za kulipia na hivyo kupunguza idadi ya magari na hivyo kupunguza msongamano,” aliongeza.
Mbunge huyo pia aliitaka Wizara ya Ujenzi kuhakikisha inaitendea haki barabara ya Uhuru kwani inatia aibu.
Alisema inashangaza barabara hiyo, ambayo ipo katika Jimbo la Ikulu, imekuwa na mashimo na haifai kiasi kwamba magari yanakwama.
Kwa upande wake, mbunge wa Ludewa (CCM), Deo Filikunjombe alisema Waziri wa Wizara ya Ujenzi, Dk. John Magufuli hayumo katika mawaziri wanaodaiwa kuwa ni mizigo kwani anachokifanya kinaonekana.
Alisema endapo Tanzania ingekuwa na mawaziri watano kama Dk. Magufuli, ingefika mbali kwani amekuwa akifanya kazi zake kwa umakini mkubwa.
Filikunjombe alisema ni vyema waziri huyo akaendelea na utaratibu wake wa kujenga barabara katika sehemu zote kidogo kidogo na si kujenga sehemu moja.
ìWanosema sijui barabara zangu za Kawe, sijui za wapi hazijengwi, hapana wewe ni waziri wa Watanzania wote, hivyo jenga hivyo hivyo kidogo kidogo kila sehemu waguswe,” alisema.
Mbunge huyo alimshukuru Waziri Magufuli kwa kuanza ujenzi wa barabara katika jimbo lake na kusema kuwa, endapo kasi hiyo ingeanza miaka ya nyuma, hivi sasa barabara zingepitika zote katika jimbo hilo.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru