Tuesday 6 May 2014

Nape: CCM ni jino kwa jino na UKAWA



  •  Kamati Kuu yatoa maagizo mazito
  •  Na Sophia Ashery, Dodoma

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kimewataka viongozi na wanachama wake kujibu mapigo ya viongozi wa Umoja wa Katiba ya Watanzania (UKAWA) kwa uzito bila kuwa na woga.

Pia kimesema kitaendelea kuwaeleza wananchi ukweli kutokana na wapinzani kuzunguka maeneo mbalimbali kuwarubuni watu ili kutimiza malengo binafsi ya kisiasa.
Katibu wa NEC ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema jana mjini hapa kuwa, CCM itajibu mapigo ya wapinzani kwa uzito ule ule na itawafuata na kufuta nyayo zao popote watakakopita kwa lengo la kuwarubuni wananchi.
Alisema maagizo hayo yametolewa na Kamati Kuu ya CCM iliyokutana mjini hapa juzi, chini ya uenyekiti wa Rais Jakaya Kikwete, ambapo alisema maagizo hayo yatatekelezwa kikamilifu.
Nape alisema kwa sasa kumezuka makundi mbalimbali, likiwemo la UKAWA, yakitumia mchakato wa Katiba Mpya kuendesha siasa chafu na kuwadanganya wananchi.
Alisema kamwe CCM haitakaa kimya na kuwaacha wahuni wachache kuendelea na tabia chafu zenye mwelekeo wa kuzusha migogoro nchini.
“Tutajibu mapigo muda wowote na kwa uzito ule ule, ambao watatumia kuwadanganya wananchi.
Hatuwezi kukaa kimya na kuwaacha wahuni wachache waendeshe siasa chafu zenye kuvuruga nchi. 
“Watu wanatumia mchakato wa Katiba Mpya kutengeneza vikundi na kuwadanganya watu kwa kutumia kinga hiyo. CCM itasimama na kusema ukweli pale watakapopita kusambaza uongo wao,” alisema Nape.
Aliongeza kuwa wajumbe wa UKAWA walitoka nje ya Bunge kwa hiyari yao na hawapaswi kuwadanganya wananchi kwa kuwa Bunge ndilo chombo cha kutunga sheria.
“Kama ni wakati wa kwenda mtaani kwa ajili ya Katiba, muda bado. Lakini wakiendelea kupita huko kudanganya wananchi, basi tutawafuata huko huko na kuwaeleza wananchi ukweli wa mambo,” alisema Nape.
Alitumia fursa hiyo kuwaasa Watanzania wawe makini na kundi hilo na mengine yenye mwelekeo huo kwani, hawana nia njema na taifa na wamejipanga kuvuruga mchakato huo.
CC YARIDHISHWA NA MCHAKATO
Kuhusu mchakato wa Katiba, Nape alisema Kamati Kuu ya CCM imeridhishwa na mwenendo wa mchakato wa upatikanaji wa Katiba mpya.
Pia imewapongeza wajumbe wa Bunge Maalumu la Katiba na makundi mengine kwa kuonyesha uzalendo wa kuhakikisha maslahi ya taifa yanalindwa ili katiba ipatikane.
“Tunawaomba na kuwasihi Watanzania kuvumilia katika wakati huu wa mchakato wa upatikanaji wa katiba na tunaamini katiba itapatikana kwa muda na wakati uliopangwa,” alisema Nape.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru