Tuesday 10 September 2013

Pinda awapa ‘ofa’ Wachina


Na Mohammed Issa
SERIKALI imeiomba China ijenge viwanda vingi nchini, ili bidhaa zinazozalishwa huko, zizalishwe na Tanzania.
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, aliyasema hayo jana katika ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam, alipofungua maonyesho ya China.
Alisema wakati umefika kwa serikali ya nchi hiyo kujenga viwanda Tanzania ili kutoa fursa ya wafanyabiashara kununua bidhaa hapa hapa badala ya kuzifuata China.
Pinda, alisema bidhaa za China ni nzuri na zina ubora tofauti na inavyoelezwa.
“Tunawaomba wenzetu hawa waje wajenge viwanda vingi zaidi ili bidhaa zote zinazozalishwa huko, sasa zianze kuzalishwa hapa kwetu.
“China inatoa bidhaa nzuri, zenye ubora tofauti na hao wanaosema kuwa bidhaa zao si bora...wafanyabiashara wetu wanaokwenda China watuletee bidhaa ambazo ni nzuri,” alisema Pinda.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Abdallah Kigoda, akizungumza katika hafla hiyo, alisema dhamira ya serikali ni kuongeza viwanda nchini ili kukuza uchumi wa taifa.
Alisema tayari serikali ya China imeonyesha nia ya kuwekeza kwenye sekta ya viwanda na kwamba, baada ya muda, bidhaa nyingi zitakuwa zinazalishwa nchini.
Dk. Kigoda, alisema changamoto iliyopo ni ushindani wa soko, ambapo bidhaa nyingi zinazotoka China zinauzwa kwa bei nafuu tofauti na zinazotoka nchi nyingine.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru