Thursday, 26 September 2013

Mtanzania mwingine afa na dawa za kulevya

Na Mwandishi Wetu
MTANZANIA Moza Gaza (25), amefariki dunia baada ya kutumia dawa za kulevya aina ya Cocaine aliyokuwa amechanganya na pombe kali.
Moza amefikwa na umauti ikiwa ni siku tatu, baada ya mfanyabiashara Rajabu Rajabu mkazi wa Ilala, kufariki dunia baada ya pipi 33 za Heroine kumpasukia tumboni.
Kwa mujibu wa taarifa zilizothibitishwa na polisi wa India, marehemu Moza na rafiki yake wa kiume ambaye hajafahamika, walikwenda kwenye sherehe iliyohudhuriwa na Wanaigeria.
Polisi walisema sherehe hiyo ilifanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Stallion, katika eneo la Safdarjung Enclave, karibu na soko la Green Park Kusini mwa Delhi.
Taarifa hiyo ilisema Moza alikuwa anaishi na rafiki yake huyo ambaye hajafahamika katika eneo la South Extension II, na kwamba alianguka kwenye sherehe hiyo baada ya dawa alizokuwa amemeza kumzidi.
Hata hivyo, polisi walisema marehemu Moza alikimbizwa katika hospitali ya Sukhmani, na alifariki muda mfupi baada ya kufikishwa katika hospitali hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo ya polisi wa India, ripoti za kitabibu na maelezo kutoka kwa mashuhuda, marehemu alifariki baada ya kuchanganya dawa na pombe.
Polisi wamesema wanamshikilia meneja wa hoteli hiyo, msaidizi wake na rafiki wa kiume wa marehemu huyo kwa mahojiano na wanaendelea kumtafuta aliyeandaa sherehe hiyo.
Walisema wamefanya mawasiliano na ubalozi wa Tanzania uliopo India ili kuwataarifu ndugu zake kuhusiana na kifo cha Moza.
Mkuu wa Shirika la Polisi la Kimataifa (Interpol) Tawi la Tanzania, Gustav Babile, alisema hawajapata taarifa la tukio hilo na kwamba watalifuatilia.
Naye, Mkuu wa Kitengo cha Kupambana na Kudhibiti Dawa za Kulevya wa Jeshi la Polisi, Godfrey Nzowa, alisema hawana uhakika wa tukio hilo, na kwamba wanalifuatilia kwa karibu.
“Hili tukio bado hatujalipata kikamilifu, lakini tunalifanyia kazi ili tuweze kuelewa undani wake,” alisema.
Kwa mujibu wa Nzowa, wananchi wa India wameruhusiwa kulima Heroine kwa ajili ya matumizi ya dawa mbalimbali za kitabibu.
Hata hivyo, alisema baadhi ya wafanyabiashara, wameanza kuingiza viashiria vya dawa hizo hapa nchini kinyume cha sheria.
Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini cha Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mkumbwa Ali, hakuweza kupatikana kuzungumzia suala hilo, baada ya simu yake ya mkononi kutokuwa hewani.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru