Tuesday 17 September 2013

Utata wa kisheria watawala kesi ya 'unga' Dar


NA MWANDISHI WETU
MALUMBANO ya kisheria yameibuka kwa mara nyingine katika Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, katika kesi ya dawa za kulevya inayomkabili raia wa Kenya, Mwanaidi Mfundo au Mama Leila na wenzake wanane.
Katika malumbano hayo jana baina ya mawakili wa upande wa Jamhuri na wa utetezi, yalihusu uhalali wa notisi iliyowasilishwa mahakamani hapo juzi ya kuitwa mashahidi wawili muhimu wa upande wa Jamhuri akiwemo anayedaiwa kufunga dawa hizo.
Washitakiwa wengine ni  Anthony Karanja na Ben Macharia (Wakenya) na Watanzania Sara Munuo, Almas Said, Yahya Ibrahim, Aisha Kungwi, Rajabu Mzome na John William. Washitakiwa hao wanadaiwa kuingiza nchini dawa za kulevya aina ya cocaine zenye thamani ya sh. milioni 225.
Kabla ya kuanza kwa malumbano hayo jana, Jaji Grace Mwakipesile, alitoa uamuzi juu ya maombi ya Wakili wa Serikali Mwandamizi, Prosper Mwangamila, aliyoyawasilisha juzi wakati kesi hiyo ilipotajwa kwa ajili ya kuanza kusikilizwa.
Juzi, Mwangamila aliiomba mahakama kuahirisha shauri hilo hadi jana ili aweze kuwasilisha notisi ya kumuongeza shahidi wa ziada Betha Mamuya ambaye ni muhimu kwani ndiye aliyefanya uchunguzi wa dawa za kulevya na kufunga dawa hizo.
Ombi hilo lilipingwa na mawakili wa utetezi wakiongozwa na Yassin Memba kwa madai kwamba, hakuna sababu za msingi za kuahirishwa usikilizwaji wa shauri hilo na kwamba kwa kuwa upande wa Jamhuri ulidai una mashahidi wawili hivyo waendelee.
Memba alidai hakuna sheria inayoelekeza shahidi fulani asitoe ushahidi kabla ya mwingine. Kutokana na hali hiyo, Jaji Grace aliamua kuahirisha shauri hilo hadi jana kwa kutoa uamuzi.
Katika uamuzi wake jana, Jaji Grace alikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri la kuahirisha shauri hilo ili shahidi Betha awe wa kwanza kutoa shahidi.
Baada ya kutolewa uamuzi huo, Wakili Mwangamila alidai waliwasilisha hati ya kuitwa kwa mashahidi wa ziada Betha na Mrakibu Msaidizi wa Polisi (ASP)  Neema ili aende utoa ushahidi kwa madai kuwa Betha ni shahidi wa msingi kuanza kutoa ushahidi wake.
Hata hivyo, mawakili wa utetezi walipinga kauli ya upande wa Jamhuri kwa madai kuwa juzi walieleza wanatarajia kumuita Betha, lakini ndani ya dakika chache kabla ya kutolewa uamuzi, walipewa notisi ambayo imetaja jina la mtu mpya ambaye ni ASP, Neema.
Wakili Evod Mmanda, alidai wamepewa notisi hiyo muda mfupi kabla ya kuingia mahakamani na upande wa Jamhuri uliwasilisha notisi hiyo kabla ya kutolewa uamuzi.
"Jana (juzi), upande wa Jamhuri uliomba ahirisho ili uweze kupata nafasi ya kuwasilisha notisi mahakamani ya kumuita shahidi wa ziada Betha Mamuya. Ina maana notisi ilitakiwa iwasilishwe leo (jana), baada ya kutolewa uamuzi. Kwa maana hiyo kisheria hakuna notisi mahakamani. Notisi halali ni ile itakayowasilishwa baada ya uamuzi," alidai Mmanda.
Alidai hakuna notisi ya kuita mashahidi wa ziada na kama mahakama itaona ni notisi basi ione upande wa utetezi wamepewa wakati ambao si muafaka.
Naye Wakili Johnson Jamhuri alidai akiwa wakili wa utetezi hajakabidhiwa notisi hiyo, hivyo kunaonyesha haipo.
Akijibu hoja za mawakili hao, Wakili Mwangamila akishirikiana na Wakili wa Serikali Hamidu Mwanga, walidai jukumu la kukabidhi upande wowote nyaraka kutoka mahakamani katika kesi za jinai si la kwao ni la wahudumu wa mahakama.
Kuhusu uhalali wa notisi, Mwangamila alidai upande wa utetezi unajichanganya kwa kauli zao, hivyo aliiomba mahakama kuiona notisi hiyo imeletwa kwa wakati muafaka.
Baada ya kusikiliza malumbano ya kisheria, Jaji Grace alisema atatoa uamuzi mdogo keshokutwa na kuamuru washitakiwa kurejeshwa rumande.
Wakati washitakiwa wakitolewa mahakamani kupelekwa mahabusu walikuwa wamejifunika vitambaa kichwani kuficha
sura zao kukwepa kupigwa picha, ambapo mmoja wao alijaribu kutaka kumpiga mpigapicha.

Kuna Maoni 0 mpaka sasa.

Toa Maoni Yako Kwa Uhuru